The House of Favourite Newspapers

Mambo Makubwa ya Kukumbukwa 2021

0

HATIMAYE mwaka 2021 unakaribia ukingoni; bado takriban siku 20 tu, lakini kuna mengi yamejiri katika safari hiyo yenye milima na mabonde. Yapo ya kufurahisha na yapo ya kuhuzunisha.

Kupitia IJUMAA SHOWBIZ, kuelekea kuufunga mwaka 2021, tutakuwa tunakuletea makala za kufunga mwaka na leo tutaangazia mambo kumi (10) yaliyotikisa Bongo kwa upande wa burudani na yatabaki kukumbukwa;

 

KIFO CHA JPM

Machi 17, mwaka huu tasnia ya burudani iligubikwa na huzuni kubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Pombe Magufuli ambaye alikuwa karibu na wasanii na walipenda kumita JPM.

Ni wazi wasanii watamkumbuka kwa mambo mengi aliyowafanyia kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano aliyokuwa madarakani.

 

Wasanii waligeuza ngoma zao za mapenzi na kutia maneno ya kisiasa kwa kumsifia enzi za utawala wake, lakini baadaye, baada ya kifo, walitunga ngoma nyingi za kuomboleza kifo chake.

Ngoma ziliimbwa na karibu kada zote za wasanii kuanzia Bongo Fleva, Taarab, Singeli, Dansi hadi Gospo.

 

SAKATA LA BABA WA DIAMOND

Mama mzazi wa Diamond Platnumz, Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote, Januari 29, mwaka huu aliibuka na kudai Mzee Abdul Juma siyo baba halisi wa msanii huyo kama inavyofahamika, bali ni Salum Nyange. Sakata hilo lilibamba vyombo vya habari na baadaye Mzee Abdul akakubali yaishe kisha akapiga marufuku Diamond kutumia jina lake. Sakata likaisha kiaina na hadi sasa Diamond analitumia jina hilo.

 

NDOA YA LULU NA MAJIZZO

Hili ni tukio lililokuwa linasubiriwa kwa kipindi kirefu ndani ya kiwanda cha burudani Bongo. Hii ni kutokana na wawili hao kuwa katika uchumba kwa kipindi cha muda mrefu.

 

Mwigizaji Lulu na C.E.O WA EFM, Majizzo walifunga ndoa Februari 16, mwaka huu katika Kanisa la St Gasper lililopo Mbezi-Beach jijini Dar. Tofauti na mastaa wengi, harusi ya Lulu na Majizzo ilifanyika kwa kujumuisha ndugu na marafiki wa karibu pekee na mapaparazi ilibidi wafanye kazi ya ziada kubaini tukio hilo.

 

WASAFI TV KUFUNGIWA

Mapema Januari 6, mwaka huu, Televisheni ya Wasafi inachomilikiwa na Diamond Platnumz ilifungiwa miezi sita na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufuatia kukiuka kanuni za maudhui kwa kumuonesha msanii Gigy Money akinengua jukwaani akiwa nusu utupu.

 

Hata hivyo, adhabu hiyo ilikuja kupunguzwa na Wasafi TV kuruhusiwa kurejea hewani Machi Mosi, mwaka huu mara baada ya kukiri kosa na kuomba kupunguziwa adhabu hiyo.

 

ALBAM KIBAO

Hakuna ubishi mwaka huu wa mwaka 2021 umevunja rekodi ya miaka 10 na zaidi iliyopita ambapo wasanii wa Bongo Fleva wametoa albam pamoja na Extended Playlist (EP).

 

Baadhi ya Wasanii waliotoa albam ni King Kiba (Only One King), Lady Jaydee (20), Rayvanny (Sound From Africa), Weusi (Air Weusi), Mbosso (Definition Of Love) na wengine kibao huku Nandy akiachia EP ya Wanibariki na Lava Lava (Promise).

 

GIGY NA BASATA, KENYA

Msanii Gigy Money mwaka huu ametumikia adhabu ya miezi sita ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za sanaa aliyopewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa madai ya kutumbuiza akiwa nusu utupu kwenye Tamasha la Tumewasha jijini Dodoma.

 

Akiwa bado kifungoni, Gigy alikwenda nchini Kenya kwa mwaliko wa mchekeshaji, Eric Omondi aliyekuwa anafanya tamthilia yake ya Wife Material. Hata hivyo, Gigy na Omondi walijikuta wakikamatwa na Bodi ya Filamu Kenya (KFCB) kwa madai ya kukiuka taratibu.

 

PAULA NA RAYVANNY

Katikati mwaka 2021 Februari ilisambaa video isiyo na maadili ikimuonesha Rayvanny na mtoto wa mwigizaji Kajala na mtayarishaji wa muziki, P Funk Majani wakijivinjari. Hilo liliibuka saa chache baada ya Harmonize kuweka wazi yupo katika uhusiano na Kajala.

Kusambaa kwa video hiyo kulisababisha Rayvanny kufikishwa kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar.

 

UTAMBULISHO ANJELLA KONDE GANG

Mwanzoni mwa Machi, mwaka huu Lebo ya Konde Gang Music Worldwide inayomilikiwa na Harmonize ilitangaza kumsajili rasmi Anjella na kuwa msanii wa kwanza wa kike kuwa chini ya lebo hiyo.

 

Mwimbaji huyo alikuwa ameshashirikishwa na Harmonize katika wimbo wake wa All Night.

Ikumbukwe kwamba, ujio wa Anjella unaifanya Konde Gang kuwa na jumla ya wasanii saba ambao ni Harmonize, Ibraah, Country Boy, Cheed, Killy na Skales wa Nigeria.

 

LEBO YA RAYVANNY

Rayvanny naye alifungua lebo yake aliyoipa jina la Next Level Music (NLM) na kuwa msanii wa kwanza chini ya WCB kufanya hivyo ilihali bado yupo chini ya lebo.

 

Ikumbukwe wasanii kama Rich Mavoko na Harmonize waliojitoa katika lebo hiyo kwa nyakati tofauti, nao walikwenda kuanzisha lebo zao ila Rayvanny imekuwa tofauti kwani ameanzisha lebo yake, lakini anaendelea kuitukimikia Lebo ya WCB bila taabu yoyote.

 

MATAMASHA NDANI NA NJE

Tamasha la Serengeti Music lililoanzishwa na Serikali kwa lengo la kutangaza utalii nchini lilianzia Dar mwaka jana na hatimaye makao makuu ya nchi, Dodoma ambapo lilifanyika Februari 6, mwaka huu.

 

Tamasha hili kwa mwaka 2021, likiwaweka wasanii zaidi ya 70 katika jukwaa moja. Baadaye yalifuatia matamsha mengine makubwa ya ndani kama Nandy Festival, Zuchu Home Coming, Ibraah Home Coming, Komaa Concert na mengine yaliyokusanya wasanii wengi.

 

Baada ya wasanii waliokwenda kukiwasha nje ya Bongo baada ya kupungua makali ya UVIKO-19 ni pamoja na Harmonize na Diamond (Marekani), King Kiba (Rwanda), Nandy na Zuchu (Nigeria), Rayvanny na Mbosso (Kenya) na wengineo.

 

HARMONIZE Vs DIAMOND

Ilipofika Novemba, mwaka huu, Harmonize aliibuka na mengi akitokea nchini Marekani ndipo akamtapika Diamond kuhusu mkataba alioingia na WCB akidai kwamba alikuwa akiambulia 40% ya mapato yote anayoingiza na WCB kuchukua 60%.

 

Harmonize alieleza hayo yote kutokana na watu kuwa dhana ya kwamba yeye ni msaliti. Alisema alifanyiwa fitna nyingi zilizomsababisha kuondoka kwenye lebo hiyo.

Alisema uongozi mzima wa WCB walikuwa wanamuogopa yeye (Harmonize) kwamba anaelekea kumshinda Diamond kimuziki hivyo akawa anafanyiwa kila aina ya manyanyaso.

 

Alitolea mfano safari yake ya Nigeria ambapo alikwenda kwa gharama zake kufanya kolabo na Reekado Banks, lakini aliporejea akakatwa Dola za Kimarekani 5,000 na WCB. Alipoona fitna zimezidi alijaribu kutafuta amani, lakini ilishindikana ndipo akaamua kuondoka Wasafi kwa kulipa shilingi milioni 600 ili kuvunja mkataba.

Makala; Elvan Stambuli, Bongo

Leave A Reply