The House of Favourite Newspapers

Meya Dar aitumbua kampuni ya ushuru wa maegesho ya magari

0
MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Issaya Mwita, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, leo amesitisha  mkataba na Kampuni ya Mwamkinga Auction Mart and Brokers iliyokuwa ikifanya kazi ya kudhibiti uegeshaji wa magari katika maeneo yasiyo rasmi katika Halmashauri ya Temeke na Kigamboni.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini leo, Meya Mwita amesema amefikia uamuzi huo kutokana na kampuni hiyo kufanya kazi kwa kutozingatia matakwa ya mkataba na hivyo kuanzisha migogoro isiyo ya lazima baina ya halmashauri ya jiji na wananchi.

 

Amefafanua kuwa jiji liliingia mkabata na kampuni hiyo Aprili mwaka huu kwa lengo la kufanya kazi hiyo ambapo mkataba huo ulielekeza kufanya kazi kwa weledi mkubwa, kuzingatia sheria, miongozo, maelekezo, kanuni na taratibu zilizopangiwa bila kusababisha bughudha, uonevu, kero na usumbufu kwa wananchi, jambo ambalo halikufanyika.

 

“Tumefuatilia kwa karibu sana utendaji kazi wao, kutokana na malalamiko ambayo yalikuwa yanatolewa na wananchi, tukajiridhisha kwa ushahidi uliojitosheleza. Hawawezi kunyanyasa watu na mimi kama meya wa jiji hili nikawaachia, hili haliwezekani,” amesisitiza Meya Mwita.

 

Amesema kampuni hiyo inapaswa kuondoka mara moja kwenye maeneo iliyopangiwa kufanya kazi hiyo na kuhakikisha kwamba kuanzia tarehe ambayo mkataba huo umesitishwa iwe imekabidhi mashine zote za kukusanyia mapato kwa halmashauri zikiwa katika hali salama.

 

Aidha Mwita amesisitiza kuwa hatasita kuzichukulia hatua kampuni nyingine ambazo zimepewa tenda hiyo na kuzionya kuwa iwapo wana tabia hiyo waache mara moja kwani kazi waliyopewa si ya kunyanyasa wananchi bali ni kufanya kazi kwa kufuata sheria.

 

NA DENIS MTIMA/GPL

 

Global TV Kenya: Uhuru Kenyatta Atoa Kauli Kuhusu Maamuzi ya Mahakama Kuu

Leave A Reply