The House of Favourite Newspapers

Mondi, Kiba Watajwa Amani Kongo

0

 

Mastaa wawili wa muziki kutoka nchini Tanzania wanaofanya vizuri zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ wametajwa katika hatua za kuleta amani kwenye nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Wanajeshi cha Kulinda Amani Kongo kutoka Tanzania cha TANZBATT 7, DRC, Luteni Kanali John Ndunguru, Diamond au Mondi na Kiba, wanastahili pongezi kwa kueneza Lugha ya Kiswahili ambayo hata wao imewarahisishia zoezi la kuleta amani nchini humo.

 

Katika mazungumzo yake na Ofisa wa Jeshi la Kongo (FARDC) huko Beni, Mashariki mwa Kongo, Kanali Ndunguru alisema waimbaji hao wa Tanzania wa muziki wa Kizazi Kipya na muziki wa Injili, wana mchango wao mkubwa.

 

Katika habari hiyo iliyorushwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN), wanamuziki hao wamesaidia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa Kiswahili katika nchi wanazolinda amani chini ya Umoja wa Mataifa.

 

Alizitaja nyimbo za Mondi na Kiba kwa upande wa muziki wa Kizazi Kipya na waimbaji kama Rose Muhando na Christina Shusho kwa upande wa nyimbo za Injili.

 

PONGEZI

Alisema nyimbo zao zimechangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa Lugha ya Kiswahili nchini Kongo, tofauti na lugha nyinginezo.

 

“Kuna suala moja ambalo kwa kweli naomba nilizungumze.

“Naomba nitoe pongezi zangu za dhati kwa wasanii wetu wa Tanzania, waimbaji wa nyimbo za Injili na vilevile hata waimbaji wa hizi nyimbo za Kizazi Kipya, wamechangia sana katika kueneza hii Lugha ya Kiswahili katika nchi hii na sisi imeturahisishia kazi yetu.

 

WAMO MUHAN DO NA SHUSHO

“Ukipita mitaani, utasikia nyimbo za Injili kama vile za Rose Mhando na Christina Shusho, vilevile za Kizazi Kipya kama vile za Diamond Platnumz na Ali Kiba.

 

“Sasa hivi tukipita huko mitaani, watu wakituona sisi tunapita kuzungumza nao, tunawakuta hasahasa wakizisikiliza zile nyimbo na wakituona sisi wanaona kwamba sisi ndiyo wale ambao tumekuwa tukiziimba zile nyimbo,” alisema.

 

MAT UMIZI YA KISWAHILI KONGO

Nchini Kongo, Kiswahili imekuwa nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa, ikitumiwa na walinda amani wa chombo hicho hususan wale wanaotoka Tanzania.

 

MEJA KIBIRA

Meja Michael Kibira ni miongoni mwa walinda amani mjini Beni jimboni Kivu-Kaskazini, anasema; “Lugha ya Kiswahili imekuwa ikiongelewa katika eneo la Kivu-Kaskazini.

 

“Hii sisi tunaitumia kama ni faida kwetu kwa sababu unapokuwa unakutana na raia wa Kongo, unakuwa uko huru kuongea naye, naye anakuamini.

 

“Unajua katika maeneo ya vita, yule ambaye ni mwathirika wa vita anakuwa ni mtu ambaye anatilia shaka kila mtu ambaye ni mgeni kwake.

 

“Hapa Kongo tumekuwa tukifanya kazi na mataifa mbalimbali kama Malawi, Afrika Kusini na Indonesia.” Anasema mlinda-amani huyo.

 

Anatoa mfano zaidi; “Kwa mfano hapa ninafanya kazi na mtu kutoka Indonesia, kwa hiyo wakikutana na mtu ambaye ni raia wa Indonesia, ni tofauti kabisa na wanavyokutana na sisi kwa sababu wanapokutana na mimi, wanakuta sihitaji kuwa na msaidizi wa lugha.

 

“Kwa hiyo, tunatumia Kiswahili kama silaha ambapo naweza nikaambiwa kitu kama akiona adui anakwambia kule rafiki usiende kuna hii na hii, kwa hivyo mimi nasema hiyo ni silaha na msaada mkubwa sana kwetu Watanzania, hapa Kongo,” anasema Meja Kibira.

 

KEPTENI LIHEGA

Kwa upande wake Kepteni Salum Lihega anasema, lugha ya Kiswahili inafanikisha doria; “Lugha ya Kiswahili imetoa msaada mkubwa sana kwetu kwa sababu imeleta urahisi sana katika kuwafikia raia na kufanya nao mazungumzo mbalimbali.

 

“Lugha ya Kiswahili imeenea na hii imetuletea urahisi sana katika kuwafikia raia, kuzungumza nao, kupata taarifa mbalimbali na pia sisi kujenga nao uhusiano wa karibu. “Kuna suala moja ambalo kwa kweli naomba nilizungumze kwa dhati kwa wasanii wetu wa nyimbo za Injili na vilevile waimbaji wa nyimbo za Kizazi Kipya, kiukweli wamechangia sana kueneza Kiswahili,” anasema.

 

Walinda amani hao kutoka Tanzania wanaendelea kuelezea ni kwa vipi wakiwa wanasaka taarifa za ulinzi wa amani, Kiswahili ni nyenzo muhimu.

 

LUTENI MZUNGU

Luteni Godfrey Mzungu anasema; “Niko huku kwenye ulinzi wa amani katika kuongoza doria mbalimbali, nimekuwa katika jukumu hili kwa maeneo ya Beni na Mavivi, lakini pia nimekuwepo katika majukumu katika sehemu moja inaitwa Matombo.

 

“Mfano mzuri, mimi katika eneo la Sake katika doria zangu najitahidi kukutana na raia wengi tunaongea lugha ya Kiswahili vizuri, ni tofauti kati ya majirani wenzetu ambao wapo katika hili jukumu, inaleta shida sana katika kuwasiliana na raia, inafikia kipindi mpaka wawe na mtu anayetafsiri. Lakini sisi raia wanatueleza shida zao mbalimbali, tunakutana na machifu wao wanatufikishia habari mbalimbali ambazo zinasaidia kabisa katika utendaji kazi wetu.”

 

SAJINI MOHA MMED

Kwa upande wake, Sajini Nassoro Mohammed anasema; “Kiswahili kimetusaidia sana kwa ndugu zetu Wakongo kuleta umoja Kongo, kwa hiyo inasaidia sana na wanapenda sana tuongee Kiswahili na wanapenda sana lugha yetu ya Kiswahili kwamba, kumbe lugha ya Kiswahili ni nzuri kuliko hata lugha yao.

 

“Wanasema lugha yao ni ngumu kuliko Kiswahili kwa vile ni rahisi sana. Sisi kimetusaidia kuliko mataifa mengine tuliyonayo kama Bangladesh, Malawi au Afrika Kusini.”

Stori: Mwandishi wetu, DAR

Leave A Reply