The House of Favourite Newspapers

MUNGU KAWANUSURU KIFO MASTAA HAWA 2018!

“NANI kauona mwaka, tunamaliza mwaka, ni majaliwa yake Mungu kuuona mwaka! “Ingawa kuishi ni bahati na kufa ni lazima kwetu ni vizuri ndugu kupanga mikakati kuchangia kuokoa maisha yao… “Ufahari msibani na makamera ya video mazishini…Ni majaliwa yake Mungu kuuona mwaka!”

 

Hiyo ni sehemu ya mashairi ya Wimbo wa Huruma kwa Wagonjwa ulioimbwa na bendi kongwe nchini ya DDC Mlimani Park Orchestra miaka hiyo. Mashairi haya yanatukumbusha kuwa wakati zimebaki siku chache kuuaga mwaka 2018 na kuingia 2019, hakuna mwenye uhakika wa kumaliza mwaka na kuingia kwenye mwaka mwingine mpya ila yote ni kutokana na majaliwa yake Mwenyezi Mungu.

 

Mwaka 2018 haukuwa mzuri kwa mastaa watatu Bongo, Ali Choki ambaye ni nguli wa muziki wa Dansi, Hawa Said almaarufu Hawa Nitarejea wa Wimbo wa Nitarejea na staa wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ ambapo Mungu aliwatendea muujiza na kuwanusuru na kifo.

1: ALI CHOKI

Gwiji huyu wa muziki wa dansi nchini Mungu alimtendea muujiza pale alipompigania na kumwezesha kurudi mzigoni kwa kishindo na kuibuka na wimbo mpya wa Naufunga Moyo. Choki alifanikiwa kurudi kwenye gemu akitokea kitandani ambako alikuwa amelazwa akiugua maradhi ya kisukari na presha kwa zaidi ya miezi mi wili.

 

Choki alifikia hatua ya kulazwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza. Choki, baada kupita kwenye kipindi kigumu cha kuumwa akipita kwenye bonde la mauti, Mungu alimnusuru na baadaye afya yake iliimarika na madaktari wakamruhusu kurudi jukwaani. Kwa kinywa chake, Choki alikiri kupita kwenye mtihani mzito wa kuumwa na ni Mungu pekee aliyemnusuru na kifo.

2: HAWA NITAREJEA

Msanii Hawa alipata jina aliposhirikishwa kwenye Wimbo wa Nitarejea wa staa mkubwa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’. Mwaka 2018, Hawa alichungulia kaburi huku tumbo likiwa limejaa maji ambapo madaktari wa hapa Bongo walidai alikuwa akisumbuliwa na ini kutokana na matumizi ya pombe kali ikiwemo gongo na madawa ya kulevya.

 

Wakati hali yake ikizidi kuwa mbaya, Diamond aliguswa na afya ya Hawa ambapo alijitolea shilingi milioni 50. Hawa alipelekwa kwenye matibabu nchini India.

 

Akiwa India, iligundulika kuwa tatizo halikuwa kwenye ini bali lilikuwa kwenye moyo. Hawa alifanyiwa operesheni ya moyo iliyozaa mafanikio makubwa kabla ya kurejea Bongo na kumshukuru Mungu kwa kumnusuru na kifo kisha Diamond ambaye alimtolea kiasi hicho cha fedha.

 

3: OMMY DIMPOZ

Kati ya mwezi Juni na Julai, hali ya kiafya ya Ommy Dimpoz ilikuwa mbaya mno kiasi cha kutangaza hadharani ili Watanzania wamuombee. Ommy Dimpoz alianza kwa kufanyiwa matibabu nchini Kenya bila mafanikio na kushauriwa kwenda nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Awali hakuweka wazi ni ugonjwa gani hasa unaomsumbua, lakini baadaye ilibidi afunguke kuwa alikuwa amefanyiwa upasuaji wa koromeo. Ommy Dimpoz alisema kuwa alianza kuona dalili za kukaukiwa koo na baadaye alishindwa kabisa kumeza chakula wala kitu chochote mdomoni. Ilielezwa kuwa koromeo lake lilikuwa limesinyaa na kumuathiri msanii huyo kiasi cha kuhitaji operesheni.

 

Ommy Dimpoz alisema alielezwa na madaktari kuwa tatizo hilo alilipata baada ya kunywa sumu kwenye kinywaji hivyo koromeo kuvimba na kumsababishia maumivu kwenye na kushindwa kula wala kumeza kitu chochote.

 

Hata hivyo, baada ya operesheni kubwa nchini Afrika Kusini, aliporejea nchini hali ilikuwa mbaya kwa mara nyingine hivyo kulazimika kukimbizwa nchini Ujerumani kwa matibabu zaidi. Hadi unasoma makala haya, tayari Ommy Dimpoz ameruhusiwa kutoka hospitalini nchini Ujerumani na kupelekwa jijini Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya kuwa chini ya uangalizi maalum wa madaktari.

Comments are closed.