The House of Favourite Newspapers

Mzee Majuto, Snura Anakuchafua au Unajichafua Mwenyewe?

0
    Msanii wa Bongo Snura Mushi.

NI ukosefu wa heshima kwa mtu yeyote wa burudani, hasa za filamu za vichekesho, kutotambua uwezo wa muigizaji huyu bora wa miaka yote nchini Tanzania, Amri Athuman au majina yake ya kikazi, King Majuto au Mzee Majuto. Kati ya waigizaji wenye vipaji vya kweli, miongoni mwao ni huyu mzee, mwenyeji wa Tanga.


Hahitaji kupata ukumbi mkubwa uliopambwa au eneo la kifahari ili aweze kuonyesha umahiri wake wa kuvunja mbavu. Muweke popote pale, akiamua, atakupasua mbavu zako uondoke ukiwa umechoka.

 

Mpeleke vijijini, kule ndanindani kabisa, halafu muweke kwenye kijumba kidogo cha udongo, halafu kaa pembeni akupe burudani, utafurahi na roho yako. Mpandishe kwenye daladala, hata usimkalishe, asimame, lakini akianza kutoa dozi, utampisha kiti akae.

 

Ni mmoja kati ya waigizaji wenye vipaji vikubwa ambao Mungu aliwapatia Watanzania. Ni kama maini ya ng’ombe vile, hata akizeeka, yanaendelea kuwa na utamu uleule, ndivyo alivyo Mzee Majuto, hata uzeeni mwake, uwezo wake wa kuchekesha umebakia palepale.

Msanii mkongwe King Majuto au Mzee Majuto.

Tangu wakati ule akiwa na wahenga wenzake, akina Mzee Small, Mzee Jangala, Bi Chau, Pwagu na Pwaguzi, hadi leo anaposimama na vijana wadogo kama akina MC Pilipili, Idris Sultan, Steve Nyerere na wengine wa aina hiyo, anabakia kuwa mkali zaidi yao maana vitu vyake si vya kawaida.

 

Kama itatokea, hata katika maisha ya kawaida tu, ukutane na Mzee Majuto halafu muachane ukiwa hujacheka, ni lazima ujihesabu kuwa na matatizo fl ani ya kibaiolojia, kwa sababu ile kumuangalia tu, ni lazima upate kicheko. Huyu mzee anachekesha bwana, wee acha tu.

 

 

Nikiwa ni shabiki wake mkubwa, tena wa miaka mingi, nilipata faraja sana mwaka 2015, wakati mzee huyu alipokuwa miongoni mwa Watanzania ambao walikwenda hija, kule Macca kujihi, kama moja ya nguzo muhimu kwa waumini wa Dini ya Kiislamu.

 

Kwa wanaokumbuka, hija ya mwaka ule iliandamana na majanga, kwani mahujaji wengi walipoteza maisha baada ya kukanyagana, wakati wa zoezi tunaloambiwa ni la kutupa mawe. Baada ya kurejea akiwa salama,King Majuto alisema kwa kuwa sasa ni alhaj, hatajihusisha tena na uchezaji wa fi lamu zenye mwelekeo wa mapenzi, kwani akiwa ni mtu mzima na mume wa mtu, maadili yanamzuia kidini na hata kijamii. Wenye mapenzi mema na maadili ya waigizaji wetu na hasa Mzee Majuto ambaye licha ya utu uzima wake leo anaweza kucheza kama kijana wa kisasa, tulimwelewa na kumtakia mema.

 

Lakini juzikati nimeona vipande vya muziki wa video vya wimbo wa msanii Snura Mushi, yule mdada ambaye wakati fl ani pia video yake iliwahi kufungiwa, baada ya kufanya ‘kufuru’ katika Wimbo wa Chura. Katika vipande hivyo vichache, King Majuto, kwa namna ya kuwavunja watu mbavu, anafurahia mauno ya Snura.

 

Tena anafurahi hadi anajikuta anaacha kazi yake nzuri ya kupaka rangi ukuta, badala yake anampaka mtu usoni na wakati mwingine anaiacha pasi kwenye nguo hadi inaunguza nguo, kisa tu mauno ya binti wa kike! Najua uigizaji ni kazi yake inayompatia riziki ya kila siku hivyo ni lazima afanye kazi ili mkono uende kinywani. Tatizo langu kwa Mzee Majuto, ni vipi sasa ile kauli yako ya kutofanya tena mambo hayo ya kidunia? Hapa simaanishi uache kuigiza, isipokuwa ningefurahi sana kwa ukongwe wake, angeishi kwenye maneno yake.

 

King Majuto si mtu wa kutafuta kiki kwa kauli zake, ni staa mkubwa kabisa ambaye kwa umri wake, anastahili kuwa mfano wa kuigwa. Utu uzima dawa. Tunategemea waigizaji wakubwa kama Mzee Majuto waendelee kubakia kuwa mfano katika maneno na vitendo. Kama mashabiki wanamlazimisha kukana maneno yake, basi arejee tena hadharani na kutupa ukweli na sisi tutamwelewa kama tulivyomuelewa pale mwanzo. Nasema hivi kwa kuwa, hadi sasa sijajua kwamba kwa video hiyo ni Snura anamchafulia Mzee Majuto au Mzee Majuto ndo’ anajikapa matope.

Leave A Reply