The House of Favourite Newspapers

Nandy ‘Ampiga’ Kiba!

0

UNAWEZAkusema ufalme wa Ali Kiba ‘Kiba’ kwenye mtandao wa YouTube ni kama umepinduliwa mapema, takwimu zinaongea.Ile kukaa tu kitini na wimbo wake wa So Hot, msanii huyo amejikuta akipigwa kumbo na Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ na ngoma yake ya Acha Lizame.

 

Takwimu za YouTube zinaonesha kuwa, Kiba aliachia ngoma yake hiyo Juni 8 mwaka huu, ambapo siku nne baadaye Nandy naye alibisha hodi.Waswahili husema “koti likipasuka hupepea” na ndivyo ilivyokuwa kwa wimbo wa Kiba uliokuwa umeshika Namba Moja, ulijikuta ukipeperushwa na ule wa Nandy na kupisha kiti cha trending za YouTube.

 

Hadi Juni 18, takwimu zilipochukuliwa na mwandishi wetu, Acha Lizame ulikuwa unashika Namba Moja ukiwa umetazamwa na watu 1,517,177 huku So Hot ukiwa umeangaliwa mara 1,533,267.

 

Kuna msemo wa “kila jambo na wakati wake” na kweli kuna wakati wa kulia na ule wa kucheka, kama Kiba alivyocheka alipoushusha wimbo wa Quarantine wa Wasafi kutoka Namba Moja, naye amejikuta akilizwa na Nandy ambaye kwa sasa anacheka mpaka basi.

 

Siku za hivi karibuni mnyukano wa wasanii umehama kutoka kwenye shoo za majukwaani hadi kwenye mitandao ya kijamii, ambako mbali na kuwafikia mashabiki wengi sehemu mbalimbali duniani kwa wakati mmoja, lakini kuna fedha za mtandaoni ambazo wasanii hulipwa kutokana na kazi zao kufanya vizuri.

 

Kwa msingi huo, mafanikio kwenye mitandao ya kijamii, limekuwa jambo linalowafurahisha wasanii wengi, sawa na kupata shangwe za majukwaani kwenye shoo.

 

Aidha, siku chache baada ya Nandy kumpiga kumbo Kiba, naye amejikuta akikabwa koo vilivyo na msanii Abdul Rajabu ‘Harmonize’, ambaye ameachia ngoma iitwayo Wife akimshirikisha msanii mkongwe Lady Jay Dee.

 

Kama ilivyokuwa kwa Kiba “raha ya kulima mpokezane majembe,” Nandy naye baada ya kicheko chake, amejikuta akilizwa na Wife wa Harmonize, ambao aliuachia Juni 17, mwaka huu.Hata hivyo, mwanamuziki mkongwe wa Dansi nchini John Kitime anasema katika mahojiano na mwandishi wetu hivi karibuni kuwa, muziki wa sasa wa Bongo Fleva ni kama bazoka unawahi kuisha utamu.

 

“Kuna nyimbo zimetungwa mwaka 1961, lakini hadi leo zinasikilizwa na kupendwa lakini hizi za vijana wa leo, ni tamu kwa wiki moja tu, baada ya hapo zinachuja,” alisema Kitime.

Leave A Reply