Professa Jay; Mheshimiwa asiyekubali kuacha muziki

PROF JAYMwana Hip Hop mkongwe Bongo, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ hatimaye wiki hii alifanikiwa kunyakua kiti cha Ubunge wa Jimbo la Mikumi, Morogoro kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho alikuwa akiwania na mgombea kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) bwana Jones Estomih Nkya.

Ushindi huo wa Professa Jay unalifanya Bunge la Tanzania kuwa na wanamuziki wawili wakongwe akiwemo Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ametetea nafasi yake ya Ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

Gazeti hili liliamua kumtafuta                                             Professa Jay na kuzungumza naye juu ya mipango aliyonayo ndani ya jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano cha ubunge wake.

Mwandishi: Umepata nafasi uliyoitaka kwa hamu, nini mipango yako kwa wana Mikumi?

Professa Jay: Kitu cha kwanza kabisa nilichopanga kufanya ni kuwaunganisha wana Mikumi wote. Najua walionichagua si wana Chadema tu bali hata wa vyama vingine, wameniamini, hivyo kitu cha kwanza ni kuwaunganisha na kuwakumbusha kwamba wao ni wamoja.

Mwandishi: Tatizo la maji limekuwa sugu sana Mikumi, unawaahidi nini wananchi katika hili?

Professa J: Nitahakikisha Jimbo la Mikumi linakuwa na maji safi na salama. Watu wamekuwa wakitumia maji ya visima, na hata yale safi yanayopatikana si kwa wingi kama inavyotakiwa, hivyo nitahakikisha kwamba maji safi na salama yanapatikana kwa wingi.

Mwandishi: Kuna lolote unaweza kuzungumzia kuhusu elimu jimboni kwako?

Professa Jay: Kuna tatizo kubwa la elimu. Nitahakikisha naleta elimu bora na si bora elimu, ili elimu bora ipatikane ni lazima muwe na walimu wazuri, vitendea kazi vingi vya kufundishia lakini vilevile ni lazima tuwe na vitabu vya kutosha. Shule nyingine hazina vitabu vya kutosha, kama hali itakuwa hivyo, hatutokuwa na elimu bora, hivyo nitahakikisha vitabu vinapatikana na walimu wenye ujuzi wanaongezeka.

Mwandishi: Majimbo mengi yamekuwa na tatizo la afya, kwako utalitatuaje hili?

Professa Jay: Nitahakikisha afya inapewa kipaumbele pia. Tuna hospitali lakini hatuna madaktari wa kutosha, wanazidiwa nguvu na idadi kubwa ya wagonjwa, nitahakikisha madaktari wanakuwa wa kutosha lakini pia dawa ni kitu muhimu. Nisingependa tena kuona hospitali zinakosa dawa, nitahakikisha dawa zinapatikana vya kutosha.

Mwandishi: Ajira za kutosha hakuna, utafanyaje kulitatua hili jimboni mwako?

Professa Jay: Watu wasiokuwa na ajira ni wengi sana mitaani. Hili ni janga la taifa lakini ndani ya jimbo langu nitahakikisha kwamba ajira zinapatikana. Nitahakikisha nashirikiana na wananchi kuanzisha miradi mbalimbali na kuwaajiri vijana, pia nitahakikisha kunakuwa taasisi za mikopo kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali na hata wale wanaotaka kufanya ujasiriamali.

Mwandishi: Utaendelea na muziki au ndiyo mwisho?

Professa Jay: Siwezi kuacha muziki, nimekulia kwenye muziki ila kwa sasa sitokuwa nikipiga shoo kama zamani kutokana na majukumu mengi jimboni. Nitawaangalia vijana wenye kipaji cha muziki jimboni, hao, nitahakikisha wanakua kimuziki, hata studio yangu ya Mwanalizombe nitaitoa Dar na kuileta Mikumi ili vijana wa huku wanufaike kimuziki. Kama muziki ndiyo ulionitoa, basi sitoweza kuuacha mpaka kifo.


Loading...

Toa comment