The House of Favourite Newspapers

Serikali Yasisitiza ni Kosa Kisheria Kwenda na Mtoto Baa au Kumbi za Burudani

0
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo, akifungua semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari Waandamizi juu ya masuala ya kijinsia na haki za binadamu, iliyofanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, hivi karibuni.

 

WALE wanaopenda kwenda na watoto sehemu za starehe kama baa na kwenye kumbi za burudani wakidhani kuwa wanawafurahisha watoto wao, serikali imesisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

 

Hayo yamewekwa wazi na Mshauri wa Masuala ya Kijinsia, Dk Geofrey Chambua katika Semina ya Wahariri na Waandishi wa Habari Waandamizi juu ya masuala ya kijinsia na haki za binadamu iliyofanyika hivi karibuni kwa siku mbili kwenye Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha.

Nyuma kushoto ni Mhariri wa Global Publishers, Ezekiel Kitula, akifuatilia semina hiyo. Aliyesimama ni mchangiaji na wengine pichani ni wahariri pamoja na waandishi wakifuatilia

 

Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria (MoCLA), Dk Chambua alisema sheria hiyo imewekwa kwa ajili ya maslahi bora ya mtoto.

“Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Mtoto akienda baa anajifunza nini?” alihoji Dk Chambua.

 

Mshauri huyo wa masuala ya kijinsia na haki za binadamu, alisisitiza pia kuwa ni kosa kisheria kuweka picha ya mtoto mitandaoni.

 

“Ni marufuku kuweka picha ya mtoto mitandaoni. Wazazi wengi wamekuwa wakijisikia fahari kuweka picha za watoto wao kwenye ‘status’ za mitandao yao ya WhatsApp, Instagram, Facebook bila kujua kuwa wanatenda kosa kisheria.

 

“Sheria zinazolinda haki za watoto, zinatoa katazo hilo kwa kuwa mtoto anakuwa hajatoa kibali (consent) picha yake kurushwa mitandaoni. Kwa sababu anakuwa bado ni mtoto, kwanza unamrusha ili iweje?

 

“Pia mtoto anakuwa hana utashi wa kisheria, hivyo hawezi kujitetea. Sheria zote hizi zimewekwa kwa ajili ya maslahi bora ya mtoto,” aliongeza Dk Chambua.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo (katikati), akiwa na wahariri katika semina hiyo.

 

Awali, akifungua semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo, aliwaasa wanahabari kuwa mstari wa mbele kupinga, kutokomeza na kukemea unyanyasaji wa kijinsia.

 

Bi. Makondo alisema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu kama vile ubakaji, ndoa za utotoni, ukeketaji, ukatili wa majumbani, wajane kupokwa mali za wenza wao na mauaji.

“Katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wake katika mapambano hayo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kisheria na utoaji haki, huduma za afya, elimu, kuanzisha vituo vya huduma kwa manusura wa ukatili na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola, ikiwemo mahakamani wote wanaotuhumiwa na makosa ya ukatili,” alisema Bi. Makondo.

Leave A Reply