The House of Favourite Newspapers

Seth Umeondoka na Ndoto ya Kanumba

0

NIANZE makala haya kwa kumshukuru Mungu kwa hili. Tumeagizwa tushukuru kwa kila jambo. Ndugu na rafiki yangu, Seth Bosco, umekwenda! Nakumbuka jinsi tulivyosherehekea zawadi ya uhai hapa duniani, ulipenda kufurahi zaidi kuliko kukasirika.

 

Usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka 2012, taharuki ilikuwa kubwa ndani na nje ya Tanzania. Hakuna aliyekuwa tayari kupokea taarifa za kifo cha kaka yako kipenzi, Steven Kanumba. Kila mtu aliomba, anachokiona kwenye mitandao kisiwe kweli.

 

Nikiwa na mwenzangu, Gladness Mallya (Mwandishi wa Global) tuliamka usiku huo na tukawa watu wa kwanza kufika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kujiridhisha, kwamba taarifa za kifo zina ukweli au la? Tulichokiona kwenye mitandao ndicho ambacho tulikihakikisha kwa macho yetu, tulimkuta Kanumba amelala na hawezi kuamka tena!

 

Nchi ilisimama kwa kifo cha nguli huyo wa filamu. Tulifika mahali mlipokuwa mnaishi wewe na marehemu kaka yako, Sinza-Vatcan ambapo ndipo msiba ulipokuwa. Alfajiri ya siku hiyo, mamia ya watu tayari walishakuwa wamefika wakitaka kujua kama ni kweli Kanumba hatunaye au la.

 

Kweli sasa waliamini kwamba Kanumba hatuko naye tena duniani. Kanumba alizikwa kwa heshima, mamia ya watu walifurika akiwemo aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’ ambaye alifika msibani na kutoa pole.

 

Watu maarufu karibu wote walifika, si wa sababu tu ni muigizaji wa filamu, bali ubora wa kazi za sanaa alizokuwa anazifanya Kanumba ndiyo uliowaguswa wengi na kutamani kumzika. Kanumba alikuwa chachu ya sanaa ya filamu kuvuka mipaka ya nchi yetu.

Alikuwa na ndoto ya kuifikisha mbali sanaa ya uigizaji. Alikuwa anatamani siku moja sinema zetu zishindane na sinema za Hollywood kule Marekani. Alithubutu kushindana na Wanaigeria. Wakati huo soko la filamu nchini lilikuwa limekamatwa na mastaa wa Nigeria.

 

Wakati huo ilikuwa ni nani haangalii sinema za Kinigeria zilizokuwa na mafundisho ya dini na mila zao? Ni zile zilizokuwa zinaanza na ushirikina sana halafu mwishoni zinamalizia na neno la Mungu kama suluhisho la kumaliza uchawi na mambo mbalimbali ya kishirikina.

 

Ili kuifikia ndoto yake ya kuikamata Afrika, Kanumba aliwavuta mastaa wa Nigeria hapa nchini na kufanya nao kazi. Wanaigeria wakaanza kutujua na kutambua thamani yetu katika soko la filamu. Mastaa kama kina Mercy Johnson, Ramsey Noah na wengineo wakawa wanamiminika Bongo kuja kufanya kazi.

 

Haraka sana Tanzania ikawa juu kwa sinema na kuiacha Bongo Fleva ikiwa chini. Mastaa wakubwa nchini ambao walikuwa wakipambwa kwenye vyombo vya habari hususan Magazeti ya Global Publishers, walikuwa ni wa filamu.

 

Filamu ilikuwa filamu kwelikweli. Mastaa wake walikuwa wakipamba sherehe mbalimbali, iwe ni uzinduzi wa filamu au hata kwenye kumbi za starehe ambazo bendi mbalimbali zilikuwa zikitumbuiza. Mastaa wa sinema ndiyo waliokuwa wakipewa heshima ya kipekee pindi wanapofika.

 

Ndoto ya kuifikisha sanaa ya uigizaji kwa levo ya Afrika ni kama tayari ilishatimia. Nchi kama Burudi, Rwanda, Kenya, Ghana, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na nyingine nyingi za jirani zilishaisoma namba. Kanumba akawa anaifukuzia heshima ya Hollywood.

 

Kwa juhudi zake binafsi, alishaukanyaga mji huo wa mastaa nchini Marekani. Ndoto yake ni kuona sasa mastaa wakubwa wa sinema Marekani wanaifahamu Tanzania kupitia uigizaji. Hiyo ndiyo pekee aliyokuwa anapambana nayo. Seth alikuwa mmoja wa wasaidizi wakuu wa Kanumba katika kuifikia ndoto hiyo.

Walikuwa wakiishi pamoja. Alimshirikisha mengi. Walisoma vitabu mbalimbali pamoja, mara kadhaa alimueleza kiu yake ya kutaka kuipata heshima kutoka Marekani. Kwamba nao waitambue Tanzania kutokana na uwezo wa mastaa wake wa filamu.

 

Akiwa kwenye harakati hizo, ghafla Mungu akamuita. Kwa kuwa tayari alikuwa na Kampuni ya Kanumba The Great Film, ndoto ya kukamilisha kile alichokiacha Kanumba ikabaki mikononi mwa Seth na wasanii wengine walikokuwa chini ya kampuni hiyo akiwemo Mayasa Mrisho ‘Maya’.

 

Ikawa mchana, ikawa usiku, mwaka wa kwanza, mpaka sasa wa saba. Hawakufanikiwa kuifikia ndoto hiyo na hata kampuni taratibu ilianza kusambaratika. Hawakuweza tena kufanya yale yaliyokuwa yanahitajika kufanywa na marehemu Kanumba.

 

Seth alikuwa na maono, alikuwa na mipango ya kuisimamisha Kanumba The Great Film. Nilizungumza naye mara kwa mara enzi za uhai wake kwani mbali na kazi zetu, alikuwa rafi yangu, alikuwa mwelewa na mtu mwenye kiu ya kutaka kufanikiwa, lakini naye Mungu ameumuita kabla hajaifikia ile ndoto ya Kanumba.

 

Hatuna budi kusema kazi yake Mola haina makosa, tangulia rafiki, tangulia ndugu yangu Seth kwa mapenzi ya Mungu tutaonana tena!

Raha ya milele uwape eeh bwana na mwanga wa milele uwaangazie, marehemu Seth na Kanumba wapumzike kwa amani, amina!

MAKALA: ERICK EVARIST

 

 

Leave A Reply