The House of Favourite Newspapers

Skendo Rushwa Trafiki, Polisi Yafunguka

0

VITENDO vya kuomba na kupokea rushwa kwa baadhi ya askari vinazidi kulitikisa Jeshi la Polisi nchini, huku askari wawili katika mikoa ya Iringa na Kilimanjaro wakidaiwa kukamatwa kwa nyakati tofauti kwa tuhuma hizo.

 

MARA baada ya picha za askari wa usalama barabarani kusambaa mitandaoni zikimuonesha akiwa ameshika fedha zinazodaiwa kuwa ni za rushwa, Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa ushahidi utakapopatikana hatua zitachukuliwa.

 

Tukio la kwanza lilitokea Ijumaa ya wiki iliyopita katika mji wa Himo wilaya ya Moshi ambapo Ofisa wa Polisi mwenye cheo cha Mkaguzi Msaidizi, alikamatwa akidaiwa kupokea rushwa ya Sh20,000 ili kushughulikia dhamana ya mtuhumiwa.

 

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Frida Wikesi alikiri kukamatwa kwa ofisa huyo, lakini akakataa kuingia kwa undani akisema bado ofisi yake inaendelea na uchunguzi.

 

Tukio la pili ni la Askari wa usalama barabarani wa Mkoa wa Iringa, anayedaiwa kukamatwa na fedha anazodaiwa kuzikusanya kama zao la rushwa kutoka kwa madereva na wamiliki wa magari Januari 18, 2022.

 

Picha za tukio la kukamatwa kwa askari huyo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii juzi jioni, zikionyesha ndani ya gari kukiwa na noti za Sh1,000, Sh2,000, Sh5,000 na Sh10,000 zilizokunjwa na nyingine askari mmoja akiwa amezishika baada ya kuzipanga.

 

Kufuatia tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alilieleza Mwananchi hatua za kijeshi zinaendelea kuchukuliwa.

 

“Katika mitandao ya Kijamii kumeonekana picha zinazomuonesha Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani akiwa ameshika fedha mkononi na picha nyingine ikionesha fedha zikiwa ndani ya gari kwenye koti huku picha hizo zikiambatana na ujumbe unaosema ‘Askari akamatwa akiwa na pesa za rushwa.

 

“Polisi nchini inapenda kueleza kuwa mara tu picha hizo zilivyoanza kusambaa hatua zilianza kuchukuliwa kwa kushirikiana na Wadau wengine, pia tunatamka kuwa hakuna aliye juu ya sheria hivyo hatua kali na stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na ushahidi utakaopatikana zitachukuliwa,” kauli ya Jeshi la Polisi.

 

Leave A Reply