The House of Favourite Newspapers

Stars Yapambana Yachapwa 2-0 na Zambia CHAN

0

   HUKU Taifa Stars ikianza na wachezaji wengi ambao hawana uzoefu kwenye michuano ya kimataifa, jana ilichapwa mabao 2-0 na Zambia.

 

Huu ulikuwa mchezo wa kwanza wa Taifa Stars kwenye michuano ya Chan mwaka huu, ambao ulipigwa kwenye Dimba la Limbe nchini Cameroon.

 

Katika mchezo huo, ambao Stars ilikuwa na wazoefu wachache, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Fei Toto na Danny Lyanga ilifanikiwa kuonyesha kiwango kizuri dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Stars ndiyo walianza kuliwinda lango la Zambia baada ya shuti kali na kiungo Fei Toto kupaa juu ya lango katika dakika ya 20 Hata hivyo, iliwachukua Zambia dakika tatu kujibu shambulizi hilo, lakini shuti la Collins Sikombe katika dakika ya 23 lilitoka nje ya lango.

 

Dakika ya 29 na 30, zilikuwa hatari kwa Stars baada ya Manula kufanya kazi nzuri ya kuokoa hatari mbili ambazo zilikuwa zinaelekezwa langoni mwake.

Hatari zaidi ilikuwa ya dakika ya 29, baada ya mshambuliaji wa Zambia, Emmanuel Chabula kupiga shuti kali akiwa ndani ya eneo la 18 lakini Manula akaokoa kwa ufundi wa hali ya juu.

 

Stars waliingia kipindi cha pili wakiwa na nguvu mpya lakini walijikuta wakifungwa mabao mawili ya haraka.

Dakika ya 64, Shomari Kapombe aliunawa mpira na mwamuzi kuamuru penalti ambayo ilipigwa na Sikombe na kujaa wavuni.

 

Dakika ya 80 ya mchezo, Stars walifanya tena uzembe na kuachia krosi kupigwa langoni mwao ambapo Chabula alipiga shuti kali na kujaa wavuni na mechi kumalizika kwa Zambia kushinda 2-0.

Sasa Stars imebakiza michezo miwili ya Kundi D, dhidi ya Guinea na Nambia ambazo zilipambana jana usiku.

Leave A Reply