The House of Favourite Newspapers

Tcra, Basata msiachwe nyuma na kasi ya Magufuli

0

tmp_21241-2_TCRA-Tanzania-250x250-800x500_c96447027KWENU Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata). Habari na poleni kwa majukumu yenu ya kila siku.

Kwa kuwa najua mpo wengi kwenye mamlaka hizo, salamu zangu za kipekee nazitoa kwa Mkurugenzi wa TCRA, Dk. Ally Simba bila kumsahau bosi kubwa wa Basata, Godfrey Mngereza.

Naamini wao watazifikisha kwa watendaji wote walio chini ya mamlaka hizo. Mkitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima. Namshukuru Mungu naendelea kupambana katika eneo langu la uandishi wa habari.

Madhumuni ya kuwakumbuka leo kwa barua hii, kwanza ni kuwataka kuongeza umakini katika kazi zenu na kufanya maamuzi ya haraka kuepuka malalamiko yanayoelekezwa kwenu.

Mimi natambua umuhimu wenu katika suala zima la kusimamia maadili na usalama wa nchi lakini malalamiko haya yanayotolewa na wadau mnapaswa kuyafanyia kazi zaidi ili kuzidi kujiwekea heshima.

Nasema hayo nikiwa na maana, kama kweli mmedhamiria kudhibiti kazi ambazo hazina maadili basi kweli zisipenye katika jamii na uwepo mfumo mzuri wa kudhibiti na sheria ziwaongoze kusimamia jukumu lenu.

Inashangaza kuona wimbo wa msanii unapigwa katika vituo mbalimbali vya redio, unasambaa kama njugu mitaani halafu ndani ya siku kadhaa, unasikia umefungiwa. Nyinyi wenye mamlaka mlikuwa wapi? Siku hizo kadhaa ulizochezwa mlikuwa hamuusikii? Sheria inasemaje kwa mhusika?

Elimu ya sheria zenu mmeitoa kwa wasanii? Wasanii wanajua wajibu wao kwenu? Wameuafiki wajibu wao? Wametoa mapendekezo yao? Mmewasikiliza?

Je, ni kweli mna mikakati madhubuti ya kudhibiti kazi zisizo na maadili? Tumeona wimbo wa Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, Shika Adabu Yako umepigwa kwa siku kadhaa, mkashtuka na kuufungia.

Basata; Ulifikaje redioni? TCRA; Ulirushwaje hewani? Wakati natafakari hilo, nikasikia wimbo wa Ambwene Yesaya ‘AY’, Zigo nao mmeuzuia kuchezwa mchana. Wimbo umechezwa wee hadi tukaanza kuuchoka, eti ghafla tu, mkaubana kwa maelezo kwamba hauna maadili kwa watoto hivyo uchezwe wakati watoto wameshalala.

Kwa nini mnachelewa kuupanga upigwe usiku? Mlikuwa wapi hadi wimbo ukapigwa sana mchana halafu ghafla mnashtuka kama vile mlikuwa usingizini, mnasema upigwe usiku? Hilo ni tatizo.

Kama kweli inaharibu maadili, kwa muda wote huo uliopigwa, wangapi watakuwa wameshaathirika? Wangapi watakuwa wameshaurekodi na kuucheza katika kumbi za starehe, majumbani na kwingineko bila kujali muda?

TCRA mlikuwa wapi wakati televisheni zinacheza wimbo huo. Achana na kazi za wasanii wa nyumbani, kwa nini na zile za wasanii wa nje ambazo ndizo zinatajwa kukithiri kwa kutokuwa na maadili msizuie kabisa au zipigwe nazo usiku?

Michezo mbalimbali ya kutoka nje, mnaifuatilia kwa umakini? Mnachukua hatua kwa wakati? Kama kweli tunataka kusonga mbele hatuna budi kuamka, kuacha kufanya kazi kwa mazoea, kuchukua hatua mapema, kutoa elimu ya kutosha na kuwachukulia hatua mara moja wote wanaokiuka kama afanyavyo Rais John Magufuli.

Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa.

Wenu katika ujenzi wa taifa;

………………………..

Erick Evarist

Leave A Reply