The House of Favourite Newspapers

Thea Amkana Mike Kweupe

0

KWENYE orodha ya wakongwe wa filamu Bongo ambao wanaipeperusha vizuri bendera ya Tanzania, kuna majina ambayo ni vigumu kuyaacha. Miongoni mwa majina hayo lipo la mwanamama mwenye kipaji cha aina yake, Thea.

 

Jina halisi ni Ndumbangwe Misayo almaarufu Thea. Thea alianza sanaa ya uigizaji tangu akiwa darasa la tano. Miaka ilivyozidi kwenda alijiunga na kikundi cha sanaa cha Mambo Hayo. Baada ya kundi hilo kufa ndipo akajiunga na Kundi la Kaole Sanaa.

 

Filamu kama Sikitiko Langu, Moses, Bibi Yangu, Pasuko la Moyo, Kovu la Laana, She is Mine na nyingine nyingi zilimpa umaarufu na kutambulika kwa mashabiki wa filamu ndani na nje ya Bongo.

 

Baada ya kimya kirefu, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limefanya naye mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo amefunguka mengi usiyoyajua kutoka kwake;

 

IJUMAA WIKIENDA: Hongera kwa Tamthiliya ya Ndoa Yangu, naona inazidi kufanya vizuri…

THEA: Kiukweli nashukuru sana kwa mapokezi, yamekuwa mazuri. Tulianza kuonekana Juni Mosi, mwaka huu, lakini mapokezi yamekuwa makubwa sana tofauti na tulivyotegemea.

 

IJUMAA WIKIENDA: Aidia ya Ndoa Yangu ilitoka wapi?

THEA: Siku nyingi sana nilikuwa na aidia hiyo. Pia ukizungumzia ndoa unakuwa umegusa vitu vingi sana, kwa hiyo nikaona ni vyema kama nikifikisha ujumbe kwa jamii, kuelezea changamoto na raha za ndoa.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kuna uhusiano wowote wa stori ya Ndoa Yangu na maisha yako ya kweli?

THEA: (Anacheka sana) hapana, ila inawezekana vipo vitu vidogovidogo ambavyo nilichukua, kwa sababu muda mwingine ili uguse maisha ya watu na uhalisia, lazima uigize kitu ambacho una uzoefu nacho.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mastaa gani ambao umewashirikisha kwenye tamthiliya yako?

THEA: Wapo wengi sana, yupo Joan, Kojac, Johari, Bi Staa, Tiko na wengineo.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa nini umeamua kuchukua mastaa wengi wa zamani?

 

THEA: Watu wa zamani nimefanya nao kazi sana, hivyo najua viwango na ubora wao.

IJUMAA WIKIENDA: Tamthiliya nyingi wamekuwa wakihusisha wasanii wa Bongo Fleva ili kubadili ladha, vipi kwa upande wako?

 

THEA: Sijawaza kabisa na wala sifikirii kwenye kichwa changu kufanya kitu kama hicho, ukiona nimemuweka msanii wa muziki kwenye tamthiliya yangu, basi ujue ana kipaji.

IJUMAA WIKIENDA: Mnashuti ‘season’ ya pili sasa, je, kutakuwa na jumla ya season ngapi?

 

THEA: Kutakuwa na season tano ambapo kila season itakuwa na episode 52.

IJUMAA WIKIENDA: Mbali na kucheza kwenye tamthiliya hii, umekuwa muongozaji, je, unapitia changamoto gani?

 

THEA: Sidhani kama napata changamoto, naomba niwe mkweli kwamba watu ambao ninafanya nao kazi wanajielewa.

IJUMAA WIKIENDA: Ugumu upo wapi katika kuongoza tamthiliya na filamu?

 

THEA: Tamthiliya ina ugumu wake kwa sababu yenyewe inaonesha vitu kwa undani, muvi unaweza ukachukua kitu cha miaka mitano ukakionesha ndani ya saa mbili.

IJUMAA WIKIENDA: Mbali na televisheni, kuna sehemu nyingine ya kuipata Ndoa Yangu?

 

THEA: Ndoa yangu tayari ipo YouTube, ule msimu wa kwanza, hivyo kwa watu ambao wanataka kuitazama waingie YouTube.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kweli soko la tamthiliya linalipa kuliko filamu?

 

THEA: Ni kweli, ndiyo maana watu wengi sasa hivi wanafanya tamthiliya.

IJUMAA WIKIENDA: Unaamini bifu zinasaidia kukuza sanaa?

THEA: Mimi sidhani kama bifu zinakuza, lakini ninachoamini ushindani ndiyo unakuza sanaa.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mbali na Tamthiliya ya Ndoa Yangu, unaigiza tamthiliya nyingine, je, unaugawa vipi muda wako?

THEA: Uzuri watu ambao ninafanya nao kazi ninawaeleza kabisa kuwa nina kazi nyingine, hivyo mtu akinihitaji hata sasa hivi nampa ratiba yangu, hivyo kufanya kazi kwa staili hii kwangu ni rahisi.

 

IJUMAA WIKIENDA: Teknolojia imesaidia vipi kukuza sanaa ya filamu?

THEA: Imesaidia kwa sababu zamani watu wengi tulikuwa tunatumia mfumo wa CD, lakini siku hizi ule mfumo umekufa, imekuja teknolojia ya mitandao na hata flashi, japokuwa kwa upande mwingine imeathiri hasa kwa walio vijijini na wasiojua matumizi ya mitandao.

 

IJUMAA WIKIENDA: Umewezaje kuilinda hadhi yako tangu zamani hadi sasa? THEA: Kila mtu ana malengo yake, kuna muda unafika mtu anasema anataka kutengeneza skendo fulani ili apate kitu fulani.

Lakini anasahau kwamba yeye ndiye anajua ni skendo ya kutengeneza, jamii inajua ni kweli hivyo anazidi kujiharibia.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kuna tetesi kwamba siku hizi baadhi ya wasanii hufanya kiki kwa pesa, je, kwa upande wako imekaaje?

THEA: Nimefuatwa mara nyingi, lakini sijawahi kuwaza kufanya kitu kama hicho kwa sababu ninaiona kesho yangu.

 

IJUMAA WIKIENDA: Mbali na sanaa unajishughulisha na nini?

THEA: Hakuna, kwa sasa nipo bize na kuandika na kuongoza tamthiliya.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kweli bado upo na mumeo Mike Sangu?

THEA: (Anashtuka) ni nani huyo mbona sijawahi kumsikia?

 

IJUMAA WIKIENDA: Shemeji yetu kwako, yule ambaye ulifunga naye ndoa na viapo vya kufa na kuzikana…

THEA: Simjui mtu huyo na wala sijawahi kumsikia.

IJUMAA WIKIENDA: Inasemekana ulibadili jina kwa sababu yake kutoka Ndumbagwe Misayo mpaka Salome Urassa, je, ni kweli?

 

THEA: Unajua kuna kitu watu hawakijui, sijawahi kubadilishwa jina, Salome ni jina langu halisi nilipewa na wazazi wangu na ndilo la ubatizo ila Ndumbagwe ni jina la nyumbani tu, hivyo ninayo mawili.

IJUMAA WIKIENDA: Je, upo kwenye uhusiano?

 

THEA: Hapana, bado sijawaza kuwa kwenye uhusiano wa mapenzi.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa hiyo jimbo lipo wazi?

Thea: Ndiyo…jimbo linaweza likaanza kupiganiwa (anacheka).

 

IJUMAA WIKIENDA: Unaonekana kuwa na mwili mzuri kwa sasa, je, ni nini siri ya mafanikio?

THEA: Kila kitu ni uamuzi, ukiamua kuwa mtu fulani unakuwa, mimi nimeacha kula vyakula vyenye mafuta na vitu vingine ambavyo vilikuwa vinanifanya niwe mnene, pia ninafanya mazoezi.

Makala: Memorise Richard

Leave A Reply