The House of Favourite Newspapers

Ajira Inazidisha au Inapunguza Upendo?

0

Na MWANDISHI WETU| RISASI MCHANGANYIKO| MAKALA

HAYA tena leo kama kawaida tunakutana kwenye kijiwe chetu cha kupeana somo na wakati mwingine kumwagiana makavu laivu. Juzi mjomba wenu alikuwa amealikwa kwenye pati f’lani ya marafiki ambao walikuwa wanasherehekea miaka yao sita tangu wafunge ndoa iliyokuwa na shangwe nyingi sehemu moja hivi nje ya mji.

Kulikuwa na watu kadhaa, wengi wao wakiwa mume na mke na walikuwa ni wenye umri unaoonekana kuvuka miaka 40 hivi. Kusema ule ukweli, wote tulioalikwa pale, ilionekana kama nasi tulikuwa tukisherehekea ndoa zetu, maana wengine kama sisi ndiyo tulikuwa miongoni mwa waliokula chumvi nyingi.

Kwa kuwa ilikuwa ni ‘kujichanganya pati’ yaani isiyokuwa na ratiba maalum, watu walionekana wakinywa vinywaji vyao wakihama kutoka meza moja kwenye nyingine. Mimi na mjomba wenu tulikaa na familia f’lani mbili hivi tuki-share stori.

Sasa familia moja ikaonekana baba na mama wote wameajiriwa, maana simulizi zao zilionyesha wote wanaamka asubuhi na mapema, ila kila mmoja anashika njia yake na wanaonana jioni, mama akionekana kuwa ndiye mwenye kuchelewa.

Walikuwa wanaongea kuhusu raha na karaha ya kuwa na mke anayefanya kazi ofisini, kila mmoja alichangia anavyojua kiasi kwamba tulipokuja kushtuka, na hivyo kulikuwa na wahudumu wa kutufuata na kutuletea vinywaji tunavyokunywa, tukashtukia saa nane usiku!

Sasa nikaona acha leo niwape hiki nilichokipata huko nilikokwenda nisije nikasahau, maana katika umri huu ni rahisi sana kusahau, na ukizingatia siku hizi kila kukicha kunaibuka na matukio! Mashosti, wanandoa wote kufanya kazi ofisini, kuna raha na karaha zake katika uhusiano, inategemeana na wewe mwenyewe jinsi unavyoitazama hali hiyo, akili yako ikiamini ni karaha itakuwa hivyo na ikiona ni raha, basi tena hakuna wa kuitoa!

Kijamii mashostito, baba na mama kufanya kazi ofisini ni turufu kwa familia, maana kipato kinaongezeka na hivyo kuwa rahisi kuendesha maisha. Maana mwisho wa mwezi ukifika, kilichopatikana kinawekwa mezani, mahesabu yanapigwa, bajeti inapangwa na inshaalah, akiba inahifadhiwa!

Lakini sasa, wivu ni kitu kibaya sana kinachoitafuna familia ambayo wazazi wote wawili ni waajiriwa. Kuna kutoaminiana.

Mume akiwa na mchepuko ofisini kwao au hata nje ya anakofanyia kazi, kibinadamu, hasiti kuwaza kuwa mkewe naye anafanya kama mwanamke aliyenaye, ambaye yaweza kuwa naye anatambulika kuwa ni mke wa mtu! Na wivu huu huchangiwa na tabia mpya inayozuka baina ya mama na baba, muda wa kurudi nyumbani na namna anavyorudi.

Kwa mfano, mama hakuwa mnywaji wa pombe, lakini miezi kadhaa baada ya kuajiriwa, anaanza kuja nyumbani akinuka ulabu, akiulizwa vipi, leo anasema kulikuwa na ka-fuction ofisini, mara bethidei ya staff mwenzao na vitu kama hivyo.

Baba naye anachelewa kurudi nyumbani, visingizio ni vikao kazini, mara mikutano na safari za kikazi. Haya ndiyo mambo yanayoharibu upendo ndani ya wanandoa walioajiriwa, lakini kama yakiweza kudhibitiwa, hakika, maisha ni rahisi zaidi kwa wote kuleta kipato nyumbani!

Leave A Reply