Aisee King Kiba Ameshindikana!

EEH kama bahati, sadakalawe… Nimeipata kwako…

Baby usinichukulie poa…

Mama jitete ohh…

Baby mi mti mwema…

Nipigwe mawe sababu yako…

Baby, wapinzani wananichora…

Na mi naona nimeipata…

Nimekwisha haina utaka…

Kwa kubisha uje uchukue mapipa…

Tule bata delisha…

Haina majoto haina…

Tukule mafoto kiaina…

Nikuvishe pete final…

Baby we wamoto wamoto…

You are so hot…

You are so hot…

You are hot…

You are so hot…”

Hii ni sehemu ya mashairi konki yaliyojaa utamu ulionogeshwa vilivyo na zile melodi za kiasili na midundo mizuri ya Afro-Pop.

Ni kutoka kwenye mkwaju na kichupa kipya kutoka kwa King Kiba kinachokwenda kwa jina la So Hot.

Kwa sasa, ngoma hii ndiyo habari ya mjini, watu wanatafutana balaa.

Mfalme ni mfalme tu, hawezi kulinganishwa na chochote, namaanisha kuwa, mfalme mwenyewe ni Ali Saleh Kiba almaarufu King Kiba.

Ni mwanamuziki kinara kwenye muziki wa Bongo Fleva. Achana na zile ishu za kutaka kuacha muziki na kukaa muda mrefu bila ngoma, lakini akiibuka hafanyi makosa.

Anzia enzi za Cindelera, Mapenzi Yana-Run Dunia, Mwana, Aje, Kadogo, Bembea, Mvumo wa Radi, Rhumba hadi Dodo na nyingine nyingi, zimekuwa zikitikisa na kupasua uwanda wa Bongo Fleva.

Aprili 8, mwaka huu, King Kiba aliachia mkwaju wake mkali wa Dodo ambao umefanya poa ile mbaya kwenye platforms mbalimbali kama YouTube, Tidal, Apple Music, Mdundo, Google Play, Deezer, itunes, Spotify, Boomplay, Audiomack, Amazon na kwingine kote.

Ndani ya saa chache, Dodo ilikamata ulimwengu wa burudani kwa kutazamwa na mamilioni.

Wakati Dodo ikiwa kwenye moto wake, Juni 8, mwaka huu, King Kiba ametisha tena kiasi cha mashabiki wake kutamka; “Huyu jamaa ameshindikana!”

Ngoma yake mpya ya So Hot imetengenezwa chini ya mikono ya Lebo ya Kings Music Records chini ya Kiba ambaye ndiye mkurugenzi wake.

Ndani ya siku moja, Kiba amekichafua ile mbaya na So Hot na tayari kichupa kinatrendi kwenye namba moja ikitazamwa zaidi ya mara laki tano kwa siku moja.

IJUMAA SHOWBIZ inakuletea uchambuzi wa kina wa ngoma hii ambayo sasa inasikilizwa kila kona kwa mtindo wa ku-rewind mara kwa mara.

King Kiba alipiga promo kinoma kabla ya kuiachia. Alikuwa akiwapa taarifa mashabiki wake kuwa kuna mkwaju wake mpya unakuja ambao utakuwa ni moto wa kuotea mbali.

Kweli bwana, baada ya ngoma hiyo kwenda hewani, imekuwa moto balaa.

Ndani ya saa mbili So Hot ilitazamwa zaidi ya mara laki moja na kuifanya ngoma hiyo kupanda kwa kasi hadi kufikia nafasi ya kwanza.

Kwa muda huo mfupi, So Hot imefanikiwa kuzishusha ngoma zilizokuwa zimeshikilia chati ya Mtandao wa YouTube na kuzishikisha mkia.

King Kiba alipiga ndege wawili kwa jiwe moja, maana ngoma zake zote mbili ya Dodo na So Hot zimeshutiwa visiwani Zanzibar. Ni project zilizofanywa kwa wakati mmoja.

UBUNIFU

So Hot ni ngoma ambayo imeonekana kuwa na melodi za kipekee kwani imetengenezwa na Producer Kimambo kwenye Studio za SOV.

King Kiba ameamua kunyanyua watayarishaji wanaokuja kwa kasi kwa sasa, kwani Dodo ilitengenezwa na Producer Yobo katika melodi za kiaina yake na hii mpya pia imetoka na melodi ya kitofauti. Hii ni aina fulani ya ubunifu ambao King Kiba ameamua kutumia.

Video yenyewe pia imekuwa kwenye ubunifu wa hali ya juu. Kuanzia lokesheni yenyewe kwani amefanyia katika Fukwe za Bahari ya Hindi kule Zanzibar. Watu walioonekana kwenye video hiyo, hakika wameinogesha vilivyo.

Mavazi yaliyotumika kwenye video hiyo, yameendana kabisa na aina ya mavazi yanayotakiwa kuvaliwa ufukweni. Watu walioshiriki ndani ya kichupa hicho, pia wamenogesha vya kutosha na kufanya video hiyo kuwa na muonekano wa kipekee.

MAUDHUI

So Hot ni mkwaju ambao unaomsifia mwanamke mrembo ‘Wa Moto’, akimaanisha mrembo fulani hivi mkali; yaani yuko moto.

King Kiba kwa sasa amechangamka sana, kwani amekuwa akifanya vitu kwa kutulia, hana papara katika kuachia kazi zake na ndiyo sababu imekuwa ikimfanya kukimbiza kinoma.

King amebadilika katika ladha ya muziki wake, kutokana na kuwa huru kwa kazi zake ambazo amekuwa akizipangilia vizuri.

Mashabiki walizoea kumuona King Kiba akitoa ngoma za kulia, lakini kwa sasa amechangamka sana kutokana na kubadili melodi zake kuanzia Dodo hadi hii ya sasa.

So Hot ni ngoma ambayo inachezeka, kwa sasa, kupitia ngoma hii zitakuja shoo za kutosha sana kutokana na uzuri wa kazi yake hiyo.

MASTAA WAIPIGIA

SALUTI

Mastaa mbalimbali wanaikubali ngoma hiyo akiwemo Ambwene Yesayah ‘AY’ ambaye aliiposti kwenye ukurasa wake wa Instagram na kumpongeza King Kiba kwa kile alichokifanya katika mkwaju huo mkali.

PONGEZI

King Kiba anafaa kupongezwa kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya kuanzia miaka ya 2000 hadi sasa. Bado jamaa yupo very hot kama jina la ngoma yake hiyo.

Hivyo basi, kuangusha ufalme wake ni sawa na kusubiri ndege bandarini!

 

KING KIBA AFUNGUKA +255 GLOBAL REDIO

Akizungumzia mafanikio ya ngoma hiyo ya so hot kwenye mahojiano maalum (exclusive) katika Kipindi cha Bongo 255 ndani ya Studio za +255 Global Radio kinachokwenda hewani kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 10:00, Jumatano iliyopita, Kiba alifunguka;

 

“Nimegundua dunia imebadilika. Watu walipoanza kutoa singo, wamepata mafanikio zaidi. Ndiyo maana nimeona niendelee na utaratibu wa kutoa hit song tu na ndicho nitaka chokuwa nina kifanya kuanzia sasa hivi.”

Toa comment