The House of Favourite Newspapers

Karantini Wasafi Balaa! Tale Anaswa Akipeleka Msosi

0

DAR: Karantini (sehemu maalum) aliyowekwa Rais wa Wasafi, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na memba wenzake kwa sababu ya janga la Virusi vya Corona, ni balaa, IJUMAA lina ripoti kamili.

 

Diamond au Mondi na wenzake waliwekwa karantini kwa siku 14 baada ya mmoja wa mameneja wao, Sallam Sharraf ‘SK’ kukutwa na Virusi vya Corona, hivyo Serikali kuwatenga kwa ajili ya kulinda afya yao.

 

Siku chache zilizopita, Mondi ambaye ni mkurugenzi wa lebo hiyo ya Wasafi Classic Baby (WCB), alitupia video kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram akionekana na madansa wake akiweka wazi kuwa karantini.

 

Ilielezwa kwamba, waliowekwa karantini na Mondi ni pamoja na dairekta wake wa video; Kenny, mpigapicha wake; Lukamba, Rayvanny, Mbosso, Lava Lava, mameneja wa wasanii hao na madansa wake wakiongozwa na Moze Iyobo.

 

Jambo hilo liliibua maswali mengi mtandaoni huku kila mtu akisema lake.

Baadhi ya watu walisema kuwa, inakuwaje watu wapo karantini halafu wamejikusanya sehemu moja namna hiyo?

 

Wengine wakadai kwamba, hawapo ‘siriaz’, bali wanacheza na akili za watu.

Baada ya mambo kuwa mengi na kila mtu akizungumza lake, Gazeti la IJUMAA liliamua kufunga safari mpaka sehemu wanayoishi ili kujua ukweli ambapo baada ya kufika, lilishuhudia maisha ya kifahari wanayoishi jamaa hao maeneo ya Masaki jijini Dar.

 

NI MJENGO WA KIFAHARI

Mbali na kuwa ni mjengo wa ghorofa wa kifahari, lakini pia upo ushuani na kuna ulinzi wa kutosha, hivyo haruhusiwi mtu kuingia wala kutoka zaidi ya watu wenye vibali maalum.

 

IJUMAA NA MLINZI

Baada ya Gazeti la IJUMAA kufika eneo hilo, lilifanikiwa kuzungumza na walinzi wa eneo hilo ambao walithibitisha staa huyo na kruu yake nzima kuwepo kwenye mjengo huo ambao ni ‘apatimenti’.

 

IJUMAA: Habari ya kazi?

MLINZI: Salama, nikusaidie nini?

IJUMAA: Nina shida na Diamond, nimeambiwa yupo hapa na wenzake wa Wasafi.

MLINZI: Sawa, ngoja nimtume mtu akamuite. Nimwambie anaitwa na nani?

IJUMAA: Mwambie ni mwandishi kutoka Gazeti la IJUMAA la Global.

MLINZI: Sawa. (anamtuma mtu) baada ya muda anarudi.

IJUMAA: Amesemaje?

 

MLINZI: Amesema hawezi kutoka, zungumza na meneja wake.

IJUMAA: Sawa, lakini humu wanaishi wangapi?

MLINZI: Wapo wengi, karibia kundi lao lote wapo, ila sina idadi kamili.

IJUMAA: Maisha yao kwa ujumla yakoje?

 

MLINZI: Wanaishi maisha bomba sana, si unajua tena ni watu wenye majina makubwa? Kimsingi wapo vizuri sana kwani wana kila kitu.

IJUMAA: Lakini si hatari kwa wao kuendelea kujikusanya sehemu moja?

MLINZI: Wamechukua nyumba pande mbili, pia huwa madaktari wanakuja kuwa-angalia kwa sababu wapo chini ya uangalizi maalum.

IJUMAA: Oke, sawa, kwa heri.

 

GHAFLA BABU TALE HUYU HAPA

Wakati Gazeti la IJUMAA likitaka kuondoka kwenye mjengo huo, ghafla lilimnasa mmoja wa mameneja wao; Hamisi Taletale ‘Babu Tale’ akitoka na kuwapelekea chakula mastaa hao.

Hata hivyo, Tale alipomuona mwandishi wetu, alisimama mbali naye kwa kuogopa kumsogelea.

 

Tale alisema hayupo tayari kuzungumza hadi mastaa hao watakapotoka karantini.

IJUMAA: Babu Tale heshima yako.

BABU TALE: Salama, (huku akiwa kwa mbali). Mimi siwezi kuzungumza kwa sasa, subiri mpaka tutakapotoka Karantini ndipo tutaongea, lakini pia kama mnahitaji maelezo zaidi kuhusu afya zetu, wasiliana na Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu) ndiye mwenye mamlaka hayo.

 

YATOKANAYO

Mondi na ‘kruu’ yake hiyo walikuwa kwenye ziara ya muziki Ulaya kwa muda wa wiki tatu kabla ya kurejea nchini na kutangazwa kwa janga la Corona kuingia Bongo.

Baada ya hapo, Serikali ilifanya utaratibu wa kuwaweka karantini baada ya Sallam kupatikana na Virusi vya Corona.

Mastaa hao walisafiri katika Mataifa ya Uswisi, Denmark na Ufaransa kati ya Machi 5, hadi 13, mwaka huu.

Sallam alithibitishwa kuwa na virusi hivyo baada ya kufanyiwa vipimo Machi 19, 2020.

 

Kupitia kipengele cha Insta Story kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mondi alieleza namna ambavyo anatamani janga hilo liwe ni ndoto ambayo akiamka atakuta hakuna kitu.

Aliongeza kuwa, anatamani watokee mashujaa kama wale ambao huonekana kwenye filamu na kuokoa watu dhidi ya Virusi vya Corona.

 

VIFO DUNIA NZIMA

Hadi juzi, Virusi vya Corona vinavyos-ababisha Ugonjwa wa COVID -19 vilielezwa kusababisha zaidi ya vifo 19,600 dunia nzima.

Stori: MEMORISE RICHARD, Ijumaa

Leave A Reply