The House of Favourite Newspapers

Gwajima: Spika Ndugai Ajiuzulu Awaachie Wengine – Video

0

MBUNGE wa Kawe na Askofu Mkuu wa Makanisa ya Ufufuo, Dkt. Josephat Gwajima amemshauri Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai ajiuzulu wadhifa wake huo ili awaachie watu wengine waendeshe muhimili huo muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.

 

Gwajima ameyasema hayo leo, Januari 6, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa kauli alizozitoa spika huyo, zinakwenda kuwagawa wabunge ambao wengi wanamuunga Rais Samia, jambo linaloweza kumpa ugumu katika kusimamia shughuli za bunge. 

 

Kauli hiyo ya Gwajima inakuja kufuatia kitendo cha Ndugai cha kupinga mkopo wa shilingi Trilioni 1.3 uliokopwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

 

“Nashangaa Mhe. Job Ndugai anapotoka na kusema Mhe. Rais Samia amekosea kukopa Tsh tril 1.3 wakati taarifa ya mkopo huo iliwasilishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti na kupitishwa, kama alikuwa na nia ya kukataa angekataa palepale Bungeni, hivyo ninaona kuna tatizo.

 

“Mhe. Spika Ndugai ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, kama alikuwa haridhiki na mkopo huo angejadili kwenye CC ambayo iliketi Desemba 17, 2021, Mhe. Rais yuko pale na wajumbe wako pale, kwa nini hakuuliza? Baada ya Mwezi mmoja anatoka anasema nchi itapigwa mnada.

 

“Mhe. Spika angeweza kumtafuta Mhe. Rais na kumweleza kama hapendezwi na deni la Tsh tril 1.3, ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea, ninaona kulikuwa na nia ovu.

 

“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Spika si lazima awe mwanachama wa chama cha siasa, anaweza kuwa hana chama, akagombea na kupata uspika lakini Ndugai ameingia kwa tiketi ya CCM, alikuwa anampiga Rais, mwenyekiti wake na chama kinachounda Serikali.

“Mimi namshauri bosi wangu Spika Ndugai kwa unyenyekevu kabisa, hali ni mbaya kwa sababu tayari kuna Wanachama wa CCM Bungeni ambao tutaambatana na Mwenyekiti wetu Mama Samia Hassan, atabaki peke yake na atapwaya pale Bungeni, namshauri Mh. Spika Job Ndugai ajiuzulu.

“Ndugai awaachie Watanzania wengine ambao wanamsapoti Rais Samia ili twende kule ambako kunatakiwa. Ajiuzulu ili awaachie wengine, nchi iwe salama.

“Wakati anazungumza Desemba 26, nilimwandikia ujumbe Mhe. Spika nikamwambia ‘This is Ndugai I Know’ akanijibu amechanja lakini anaumwa, siku chache baadae akatoka anaomba radhi ‘nimekosa mimi, nimekosa sana, Mungu nisamehe, Watanzania Mnisamehe, nikamshangaa.

“Haya mambo ya ‘nimekosa mimi, nimekosa sana’ yafike mwisho, sababu umekosa basi jiuzulu, lengo ni kumsaidia mama (Rais Samia),” -Askofu Josephat Gwajima.

 

Leave A Reply