The House of Favourite Newspapers

Yanga Yaiandalia Simba Mabomu Mawili

Stori: Na Wilbert Molandi | CHAMPIONI | Dar es Salaam

SIMBA na Yanga zinatarajiwa kukutana Februari 25, mwaka huu katika Ligi Kuu Bara, mchezo huo ni wa pili baada ya ule wa kwanza timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, lakini tayari presha imeanza kuwa kubwa na kuna mambo kadhaa yanazungumzwa.

Imefahamika kuwa washambuliaji nyota wa Yanga, Donald Ngoma na Amissi Tambwe wataukosa mchezo wao dhidi ya Ngaya, kesho Jumamosi kutokana na kuwa majeruhi lakini habari za uhakika ni kuwa wanapumzishwa maalum kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba.

Yanga itakipiga na Ngaya de Mbe ya Comoro lakini kwa kuwa mchezo wa kwanza Yanga ilishinda mabao 5-1 katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uhakika wa kusonga mbele ni mkubwa na hivyo mchezo ujao dhidi ya Simba ndiyo unatajwa kuwa muhimu kwao kwa sasa.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Yanga ina majeruhi wanne ambao ni Ngoma, Tambwe wenye majeraha ya goti, Obrey Chirwa (misuli) na Haruna Niyonzima (malaria).

“Yanga tayari ina nafasi ya kufuzu kucheza hatua ya pili ya michuano ya kimataifa, ni ngumu kufungwa na hao Wacomoro.
“Hivyo, viongozi tumeshauriana tuwapumzishe wachezaji wetu muhimu wenye majeraha ambao wameanza kupata nafuu kama

Ngoma na Tambwe kwa hofu ya kujitonesha kwa sababu ni wachezaji muhimu tunaotarajia wawepo mechi na Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi alisema maandalizi ya mechi yao na Ngaya yanaendelea na kikosi chao kipo fiti kwa ajili ya mapambano na wachezaji wanne wanatarajiwa kuukosa mchezo huo.

“Tunashukuru maandalizi ya mechi na Ngaya yamekamilika, kila kitu kipo vizuri na katika mechi hii tunatarajia kuwakosa wachezaji wanne kutokana na majeruhi nao ni Ngoma, Tambwe, Chirwa na Niyonzima.

“Kati ya hao, Chirwa pekee anaendelea vizuri ambaye alianza mazoezi mepesi pekee na hao wengine hawakufanya kabisa na kikubwa katika mechi hii tumepanga kupata ushindi wa aina yoyote ili tusonge mbele.

“Kikubwa tunataka bao la mapema katika mechi hii kwa lengo la kuwachanganya wapinzani wetu na ninaamini tutafanikiwa katika hilo kwani Ngaya siyo timu ya kuibeza, ni timu nzuri inayocheza soka la kujilinda sana,” alisema Mwambusi.

Aidha, katika hatua nyingine, timu hiyo jana asubuhi ilishindwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar kutokana na uwanja huo jioni kutumika kwa ajili ya mechi ya Kombe la FA kati ya Simba na African Lyon na badala yake wakaenda kujinoa Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini.

Comments are closed.