The House of Favourite Newspapers

Wema, Batuli Vita Nzito (+Video)

Wema Sepetu

Na HAMIDA HASSAN & IMELDA MTEMA| GAZETI LA AMANI| HABARI

DAR ES SALAAM: Vita mpya mjini! Waliokuwa marafiki wakubwa kabla na baada ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015 na Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ kuwa rais, Wema Sepetu na Yobnesh Yusuf ‘Batuli’ wameingia kwenye vita nzito sana kufuatia kauli ya Wema hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa mama yake mzazi, Mariam Sepetu, Sinza Mori jijini hapa hivi karibuni, Wema  alitoa kauli ya kukishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba, wasanii wanakidai pesa za ushiriki wao wa Kundi la Mama Ongea na Mwanao ‘Mom’ ambalo lilipita nchi nzima kufanya kampeni.

Yobnesh Yusuf ‘Batuli’

BAADA YA KAULI YA WEMA

Sasa, siku 5 baada ya kauli hiyo ya Wema ambayo aliitoa wakati akitokwa povu la kutangaza kukihama chama hicho na kutua Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Batuli na wasanii wenzake ambao walikuwa wote kwenye Mama Ongea na Mwanao, waliwaita mapaparazi kwenye kikao walichokifanya Hoteli ya Protea, Oysterbay jijini hapa. Kwa sasa Wema yupo Chadema akisubiri kupewa kadi na kufanyiwa utambulisho rasmi ambao unasubiriwa kwa hamu na wana Chadema wote, hasa wa jijini hapa.

YALIYOJIRI MKUTANONI

Katika mkutano huo uliochukuwa dakika 10, wasanii hao, Salome Urassa ‘Thea’, Bi Staa, Mama Nyamayao, Hertih Chumila, Tausi Mgedela, Sabrina Rupia ‘Catty’, Halima Yahya ‘Davina’, Mayasa Mrisho ‘Maya’ akiwemo na Batuli walisema hawakidai CCM na kwamba, wanashangaa Wema anaposema wanakidai chama wakati yeye ndiye aliyekuwa mlipaji.

“Sasa mimi naomba kuuliza, mtu anayelipa pesa anapokuja kusema anadai maana yake nini? Yaani alipe wenzake wote halafu yeye mwenyewe ajisahau, inawezekana kweli?” alihoji Batuli huku akionekana kuwa na hasira ambazo hazikujulikana ni juu ya Wema au alikotoka.

Mariam Sepetu na mwanaye.

Batuli alizidi kusema kuwa, Wema kusema hawakulipwa wakati walilipwa ni kumdhalilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliyekuwa msimamizi wa kundi hilo.

NJE YA MKUTANO SASA Baada ya kumalizana na wanahabari, Amani lilimtafuta Batuli na kufanya naye mahojiano zaidi ambapo alifunguka zaidi.

BATULI APEWA NAFASI YA WEMA

Msanii huyo alisema kuwa, kwa sasa yeye ndiye amechukua nafasi ya Wema kwenye Mama Ongea na Mwanao akiwa ndiye makamu mwenyekiti wakati mwenyekiti ni Steve Mengere ‘Steve Nyerere’.

Alisema: “Wema ameondoka lakini Kundi la Mama Ongea na Mwanao litaendelea kama kawaida kwani ni kama vitani ambapo akifa mmoja wengine wanaendelea.”

KATIKATI YA MAONGEZI LAZUKA JIPYA

Wakati Batuli akiendelea kuzungumza na Amani , ghafla zilifika taarifa kwamba, Wema ametupia picha yake na Batuli kwenye Mtandao wa Instagram na kusema: Huyu alikuwa rafiki yangu, tulipendana sana…

Wema katika Pozi

BATULI AMJIBU WEMA PICHA INSTAGRAM “Ulimi wako uwe wenye kusema yaliyo kweli… sema nilikupenda siyo tulipendana, nina mengi. Uzuri unanijua fika, sina tone la uoga. Kitabu chako hakina jalada leupe.”

Akawaambia waandishi: “Tutaendelea tu haya ni mapambano ndiyo kwanza yameanza. Najua Wema hawezi kunichafua kwa sababu kichwa changu anakijua, ataandika hivyohivyo kama alivyoandika mtandaoni lakini hawezi kufunguka zaidi.

“Nina uhakika nitaendelea na Mama Ongea na Mwanao kwani ndiyo kwanza itakuwa imara ingawa vishawishi vipo vingi lakini nina hakika tutakuwa imara tu huwezi kutukana kitu ambacho kimekulea na kukufikisha hapo ulipo. “Halafu mimi akaunti yangu ya Instagram ‘imehakiwa’ kwa hiyo mtu akinitaka nijali kwani sitaona. Najua leo nitatukanwa sana.”

UWOYA ANUNUA KESI

Katika hali ya kushangaza, Uwoya naye akatupia maneno yake kwenye Instagram: “Kuna vitu vinaboa sana, kada mzima unasimama hadharani na kusema ulilipwa kufanya kampeni? Unafundisha nini jamii? Kwa hiyo tuliyoyaongea kuhusu CCM wakati wa kampeni hayana maana kwa sababu tulilipwa?” Alipopogiwa simu na Amani, Uwoya alisema: “Huo ndiyo ukweli wangu.”

JIKE SHUPA AONYWA USHOGA Wakati hayo yakishamiri, shoga kipenzi cha Wema kwa sasa, Zena Abdallah, ‘Jike Shupa’ ambaye hata kwenye mkutano wa Wema na mapaparazi alikuwa meza kuu, ameonywa kuwa, asiamini urafiki wao utakata miezi kadhaa mbele.

“Halafu yule Jike Shupa hajui tu, Wema si mtu wa kufanya naye urafiki. Wameshapita wenzake kibao wakiwa marafiki wakubwa wa Wema lakini siku ya mwisho, wakaacha na ugomvi. Kuna Snura Mushi, Aunt Ezekiel, Batuli na wengine wengi, leo waki wapi?” alisema msanii mmoja ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.

Amani lilimpigia simu, Jike Shupa na kumuuliza kuhusu madai hayo ambapo alisema kwa sasa hawezi kuongea chochote. “Kwa sasa siwezi kusema lolote kuhusu hayo maneno yako, iko siku nitasema,” alisema Jike Shupa.

STEVE NYERERE ASUBIRI TENA

Kwa upande wake, mchekeshaji Steve Nyerere akizungumza na Amani kwenye Viwanja vya Leaders, Dar kuhusu matukio yaliyopita ya yeye kurekodiwa sauti na mama Wema na kutupiwa mitandaoni na kuzua taharuki miongoni mwa jamii, alisema: “Mimi kwa sasa namsubiri mama Wema au Wema mwenyewe waongee lolote halafu niseme cha kusema. Nina mengi sana, wajaribu waone kazi. “Kwanza akisema Wema kwa mfano, nitamwambia maneno fulani mwenyewe atashangaa nakwambia, yaani wasijaribu.”

AMANI LAMSAKA WEMA, MAMA YAKE Juzi, Amani lilimpigia simu Wema lakini haikuwa hewani na lilipomgeukia mama yake, simu iliita tu na alipotumiwa meseji hakujibu kitu mpaka gazeti linakwenda mitamboni

 

BATULI AFUNGUKA UKWELI KUHUSU WEMA KUHAMIA CHADEMA

Comments are closed.