The House of Favourite Newspapers

Mambo Matano ya Ajabu ya Kabila Hili ni Haya, Kabila la Wala Watu -11

Na ELVAN STAMBULI| GAZETI LA UWAZI| MAKALA

KABILA la Wakorowai linalokula watu la Visiwa vya Papua New Guinea licha ya kula binadamu wenzao wana mambo ya ajabu matano kama tutakavyoona hapa chini. Kwanza, hujenga nyumba zao juu ya miti na familia kuishi huko.

Nyumba hizo hujengwa kwa miti imara ambayo inaaminika hupakwa dawa ili isiliwe na mchwa, hivyo kuweza kudumu kwa miaka mingi. Nyumba hizo huwekewa ngazi ama za miti au kamba na wanawake na wanaume huzitumia kupanda juu kwa ajili ya kulala au kupumzika. Bila shaka waliamua kujenga nyumba zao juu ya miti kutokana na woga wa kushambuliwa na wanyama wakali wa porini.

Nyumba hizo huwa ni za miti na kuezekwa nyasi lakini hutumika utaalamu wa hali ya juu wa kutandaza miti ili watoto wao wasipate upenyo wa kutumbukiza miguu na kupata madhara kwa kuumia au kuchomoka na kuanguka chini.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni baadhi yao wamekuwa wakijenga nyumba zao chini na ni wafugaji hodari wa nguruwe na mbwa. Ajabu ni kwamba nyumba hizo huwa imara kiasi kwamba hata kama kunatokea upepo mkali, hazianguki au kuezuliwa mapaa. Pili, maajabu mengine ya kabila hilo ni kitendo chao cha sehemu za siri za mwanaume wanayemuua na kumla nyama, hupikwa supu na kupewa watu maalum kula.

Mwanamke haruhusiwi kula sehemu hizo nyeti za kiume. Tatu, wakati huku kwetu watu wanaokula nyama za watu huitwa ni wachawi, kule kwao wachawi ni wale ambao wanaamini kwamba wanaua watu kimiujiza au kuwafanya kutoweka.

Mtu akitoweka na ikadhaniwa kwamba mtu fulani ndiye aliyesababisha mtu yule kutoweka (kuwekwa msukule), mtuhumiwa hupelekwa kwa wazee wa kimila na kupewa adhabu ya mateso makubwa ili amrudishe yule aliyepotea.

Adhabu zao zilishawahi kulaaniwa na mataifa mbalimbali kwani humdhalilisha mtuhumiwa kwa kumvua nguo zote na kumning’iniza juu ya mti huku akichomwa na vitu vyenye ncha kali ili aseme amempeleka wapi yule anayedaiwa kupotea kimiujiza.

Ajabu la nne kwa Wakorowai ni kitendo chao cha kutofunika sehemu kubwa ya miili yao. Wanaume sehemu pekee wanayoithamini ni dhakari ambayo hufunikwa na kibuyu maalum huku korodani zikiachwa bila kufunikwa. Ajabu ya tano ni kwa upande wa wanawake, wao hufunika tupu zao kwa majani maalum lakini matiti huachwa wazi wakati wote na kwao hilo ni jambo la kawaida.

Wanawake wa rika lolote, hawathamini matiti yao. Wanawake pia wana maajabu mengine, husuka kamba na kujitengenezea mibebeo maalum kwa ajili ya kuwabeba watoto wao, Kamba hizo huwekwa kitu kama mfuko na mtoto kuingizwa humo na mama kumchukua kwa kuiweka kamba kichwani, hivyo kusafiri hata kama ni kwa mwendo mrefu.

Mtoto akifariki dunia huwa kuna taratibu za kimila za kumfunga na kumfunika kwa gome la mti akiwa amelala kifudifudi kabla ya kumpeleka sehemu maalum ambayo huchimbwa shimo, kisha kumrundikia kuni na kumchoma moto.

Sehemu hiyo baadaye husawazishwa na kulimwa mazao. Ajabu nyingine ni kwamba katika kijiji kimoja cha Wakorowai wakazi wana pango kubwa ambalo lina mafuvu ya vichwa ya wale wote walioliwa nyama zao na jamii hiyo.

Licha ya mafuvu hayo kuna maiti ambazo zimekaushwa, hizo ni za viongozi wao ambao wanaamini waliiongoza vyema jamii yao.

 

Comments are closed.