The House of Favourite Newspapers

Baada ya Wimbo wa Nay Kufunguliwa, na hizi nazo vipi?

Ay (kulia) akiwa na Ben Paul.

Na ANDREW CARLOS| GAZETI LA IJUMAA| SHOW BIZ

MWISHONI mwa wiki iliyopita gumzo kubwa kunako burudani hususan katika Muziki wa Bongo Fleva lilikuwa likimhusu msanii Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ na wimbo wake wa Wapo. Siku chache baada ya kuachia wimbo huo, ulimfanya kushikiliwa na jeshi la polisi kutokana na kuwepo na maudhui yanayodhaniwa kuwa ni mabaya na ya kuiponda serikali.

Licha ya kushikiliwa huko, alipigiliwa nyundo nyingine kutoka Baraza la Sanaa Taifa (Basata) kutopigwa wimbo huo sehemu yoyote. Licha ya nyundo hizo hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliagiza Nay kuachiwa huru na wimbo wake huo ufunguli- we kuchezwa sehemu yoyote. Magufuli aliongeza kuwa, amefurahishwa na wimbo huo na kutoa ushauri kwa Nay kama inawezekana aufanyie marekebisho kwa kutaja watu wengine kama vile wakwepa kodi, wauza unga, wabwia unga, wezi pamoja na watu wengine wasio na maadili katika jamii.

Ukiachilia mbali kauli hiyo ya rais, zipo nyimbo na video za Bongo Fleva zilizowahi kufungiwa na Basata kwa kile kinachoelezwa kukosa maadili huku nyingine zikipangiwa muda wa kuachiwa hewani. Kwa alichokifanya rais, yawezekana kabisa, Basata kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kupitia upya nyimbo zilizofungiwa na kuwapa muongozo wasanii hao nini kifanyike kisha kuziachia upya.

Katika makala haya nimekuchambulia baadhi tu ya nyimbo zilizofungiwa na Basata kwa kushirikiana na TCRA; UZURI WAKO – JUX Ulikuwa miongoni mwa nyimbo za kwanza za Jux ambapo video yake ilifanywa na Veno Media chini ya Director Zed Benson.

Wimbo pamoja na video yake aliachia Septemba 2013 akiwa nchini China kimasomo lakini kufikia Februari 2014 Basata kwa kushirikiana na TCRA waliufungia kwa madai ya kukosa maadili.

Snura.

NIMEVURUGWA – SNURA

Baada ya kutikisa mwaka 2013 akitokea katika tasnia ya filamu, Snura aliamua kuingia rasmi kwenye Muziki wa Bongo Fleva akiwa na Wimbo wa Majanga, wimbo na video ulifanya poa kiasi cha kumshawishi kutengeneza wimbo na video nyingine iliyoitwa Nimevurugwa.

Kwa mujibu wa Snura, alipata malalamiko kwa mashabiki wake kuhusiana na video ya kwanza ya Majanga kuwa imepoa hivyo akaamua kuja kivingine kwa kuwaoneshea mauno lakini baada tu ya kuachiwa wimbo huo wa Nimevurugwa Novemba 2013, Januari 2014, akakutana na rungu la Basata.

Madee

TEMA MATE TUWACHAPE – MADEE

Moja kati ya video kali zilizofanywa na Kampuni ya Ogopa Video ya nchini Kenya ambayo iliachiwa rasmi Januari 2014 lakini nayo kufikia Machi 2014 ikakutana na rungu la Basata kwa madai ya kukosa maadili.

Roma.

VIVA ROMA VIVA – R.O.M.A

Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 zikipamba moto na ikiwa umesalia mwezi mmoja kuelekea kupiga kura ambayo ilikuwa Oktoba 25, msanii wa Hip Hop, R.O.M.A Mkatoliki aliachia Wimbo wa Viva Roma Viva ambao ulidumu kwa wiki tatu tu na Basata kama kawaida yao wakapitisha rungu kwa madai ya kukiuka maadili sambamba na uchochezi.

ZIGO (REMIX) – AY FT DIAMOND

Baada ya kutamba na Wimbo wa Zigo Februari 2015, msanii AY ambaye ni mmiliki wa Kipindi cha Ngazi kwa Ngazi na Mkasi kinachoongozwa na Salama Jabir, alikaa kimya mwaka mzima kisha akaibuka na remix ya wimbo huo akiwa amemshirikisha Diamond Platnumz.

Salama Jabir mtangazaji wa wa Kipindi cha Ngazi kwa Ngazi na Mkasi.

Video ya wimbo huo ilifanyika Sauz chini ya Studio Space Pictures (SSP) ambao pia walihusika katika video ya MwanaFA iitwayo Asanteni kwa Kuja. Licha ya Video ya Zigo Remix kuwa na ubora wa kimataifa, TCRA kwa kushirikiana na Basata Februari 2016, waliamua kuifungia video hiyo kwa madai ya kukosa maadili.

AY alipambana lakini mwisho wa siku wakatoa ruhusa ya kuachiwa hewani kuanzia saa tatu za usiku.

SHIKA ADABU YAKO NA PALE KATI PATAMU – NAY WA MITEGO

Yawezekana ni aina yake ya uimbaji maana kati ya nyimbo tatu anazotoa mojawapo ni wazi itafungiwa na kwake hili limeonekana kama ni kitu cha kawaida. Kama utakumbuka, Nay amekuwa na matukio mfululizo wa nyimbo zake kupigwa rungu na Basata, alianza na Wimbo wa Shika Adabu Yako aliouachia Februari 2016 lakini ndani ya wiki moja tu, wimbo huo ulifungiwa kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili na uchochezi.

Licha ya hilo kupita, Julai mwaka huohuo aliachia tena wimbo mwingine wa Pale Kati Patamu ambapo kava la kutangaza wimbo huo tu lilikuwa gumzo kutokana na kuwatumia wasichana walioachia baadhi ya maeneo yao ya mwili wazi. Wimbo huo ulidumu kwa muda wa mwezi mmoja na Basata kuufungia kazi kwa kuupiga stop kwa madai ya kukiuka maadili ya sanaa na jamii kwa ujumla.

Nikki Mbishi.

I’M SORRY JK – NIKKI MBISHI

Baada ya kubamba Oktoba, 2016 akiwa na Wimbo wa Babu Talent, msanii Nikki Mbishi alifunga mwaka na Wimbo wa I’M Sorry JK lakini ulifanikiwa kudumu kwa kipindi cha miezi mitatu na kukutana na rungu la Basata. Kabla ya kuufungia wimbo huo, Basata walimuita Nikki katika ofisi zao na mara baada ya kumuachia, Nikki kwa kutumia mitandao ya kijamii aliweka wazi kusitishwa kwa wimbo huo kupigwa sehemu yoyote na atakayeendelea kusambaza asihusishwe.

Aidha, inaelezwa kuwa kufungiwa kwa wimbo huo, kunadaiwa kuwa na mistari ya uchochezi. Kama nilivyobainisha hapo juu, nyimbo hizo pamoja na video zimefungiwa na Basata kwa kushirikiana na TCRA, wito wangu, yawezekana kupitiwa upya kwa maana ya kukaa na wasanii husika na kuwapa somo la kufanyia marekebisho na kuachiwa upya kwani sanaa ni sehemu ya maisha yao.

Comments are closed.