The House of Favourite Newspapers

Kuhamia Kwake Chadema, Wema Aipasua Bongo Muvi

Na OJUKU ABRAHAM & GLADNESS MALLYA| RISASI JUMATANO| HABARI

DAR ES SALAAM: MTIKISIKO! Siku chache baada ya staa wa filamu Tanzania, Wema Abrahamu Isaac Sepetu kutangaza kukihama Chama Cha Mapindeuzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wasanii na mashabiki wa kiwanda cha filamu Bongo, wamejikuta wakigawanyika, kila mmoja akisema lake kuhusiana na ishu hiyo, Risasi Mchanganyiko lina ripoti kamili.

Wema, muigizaji mwenye mashabiki wengi nchini, mwishoni mwa wiki iliyopita alitangaza kukihama chama chake cha siku zote CCM, akitoa madai ya kutafuta demokrasia zaidi na kwamba yupo tayari kwa mapambano hayo.

Hatua hiyo hata hivyo, ilikuja siku chache baada ya kukamatwa na polisi kufuatia jina lake kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika orodha yake ya kwanza ya watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya.

KUTOKA ‘PRESS’ NYUMBANI KWA MAMA YAKE

Ijumaa iliyopita, Wema akiwa nyumbani kwa mama yake, Sinza Mori jijini Dar, aliwaambia wana habari kuwa ameamua kukihama chama ambacho marehemu baba yake, Balozi Abraham Isaac Sepetu alikuwa kada wake maarufu, kwa kile alichosema ni kutaka kudai zaidi demokrasia.

Wakati yeye akitangaza kuhama huko bila mbwembwe, mama yake mzazi, Miriam Sepetu aliwaambia waandishi hao wa habari kuwa yeye anaungana na mwanaye kukihama CCM, na kuwa ana uhakika wa wafuasi wake 5,000 nao watahama naye kuelekea Chadema, huku akitamba pia kuwa ndugu zake walio nyumbani kwao Singida, nao wameahidi kuhamia chama hicho kikuu cha upinzani.

Rich Richie na mwanaye

MKONGWE WA FILAMU, RICH RICHIE

Mkongwe wa filamu nchini, Single Mtambalike, ambaye ni maarufu kama Rich Richie, akizungumzia kitendo hicho kwa masikitiko makubwa, akihofu kuwa Wema alichukua uamuzi huo akiwa na hasira.

“Unapoamua kitu chochote ukiwa umekasirika unaweza kuja kujuta baadaye kwa vile ni uamuzi ambao haukuwepo akilini mwako kabla hujakasirika, kitu cha msingi cha kujiuliza, je, aliwahi kuupenda upande ule aliokwenda? Je, anaupenda na ataendelea kuupenda? “Watu wasifikiri kwa sababu walikipigia kampeni Chama Cha Mapinduzi, basi wao wapo juu ya sheria, hapana, mimi mwenyewe nalipishwa kodi huku hadi nasema dah, lakini hiyo ni kazi ya serikali.

Chama kinaweza kukusaidia katika matatizo kama haya lakini siyo moja kwa moja, hakiwezi kwenda mahakamani na kutaka kesi ifutwe, lakini kuna namna ambayo angeweza kusaidiwa.

“Tatizo liko moja, wakati ule wa kampeni kulikuwa na aina mbili za wasanii, waliokuwa na nia ya kupiga hela na wale makada kindakindaki kama mimi, huenda malengo yao yametimia na sasa wameamua kuonyesha rangi yao halisi.

“Sidhani kama CCM inaweza kuyumba kwa sababu ya kuondoka kwake, kabla yake walishatoka watu wazito kama Kingunge (Ngombale Mwiru), Lowassa (Edward), Augustine Mrema, lakini chama kimebaki imara. Mimi namtakia kila la kheri huko anaendako,” alisema Richie.

Thea

SALOME NDUMBAGWE MISAYO ‘THEA’

Salome Ndumbagwe Misayo ‘Thea’; muigizaji huyu maarufu wa kike naye alisema kuvunjika kwa koleo siyo mwisho wa uhunzi, kwani kabla ya Wema, watu wengi maarufu wameondoka ndani ya CCM lakini chama kimebakia na nguvu zilezile.

“Huo ni uamuzi wake binafsi na wala hakiyumbishi chama, kwani yeye ni wa kwanza kuhama CCM? Chama kitabaki imara kama siku zote, mimi wala sina wasiwasi kabisa. Kilichotakiwa kufanywa na Wema ni kushughulika na tatizo lililo mbele yake bila kukihusisha chama, sasa unataka kusema yaani wewe ufanye kila unachotaka kisa ulifanya kampeni? Hakuna kitu kama hicho.”

Jb akiwa na wapenzi wa filamu za Kibongo

JB, SHAMSA FORD WAJIWEKA PEMBENI

Mkongwe mwingine katika filamu Bongo, Jacob Stephen ‘JB’ aliipokea simu ya Risasi Mchanganyiko na baada ya kusikiliza kile anachotakiwa kutoa maoni yake, alifunguka;

“Kaka, sina comment, siyo kila kitu kinachotokea unapaswa kukizungumzia, sasa hayo mambo mimi wapi na wapi, wewe zungumza kuhusu Simba na Yanga, juzi tumewakalisha na wataendelea kukaa hadi wahame Jangwani,” alisema msanii huyo mwenye umbo kubwa.

Naye muigizaji nyota, mwenye mvuto, Shamsa Ford ambaye baada ya kuombwa maoni yake kuhusu suala hilo, kwanza aliguna na baadaye akajibu kifupi: “No Comment,” akakata simu.

Dude

KURWA KIKUMBA ‘DUDE’

Staa mwingine mkubwa katika filamu, Kurwa Kikumba maarufu kama Dude, alisema amesikitishwa na kitendo cha Wema kuhama CCM, akasema amefanya haraka, kwani alipaswa kukaa chini na kutafakari kwa kina kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa.

“Kwanza niweke wazi, mimi ninaunga mkono oparesheni hii ya kuwakamata wanaojihusisha na madawa ya kulevya kwa sababu vijana wetu wengi wanapotea, lakini pia nilitaka kuwaambia mastaa wenzangu kuwa tuache kuishi kimazoea. “Wema alifanya haraka, alipaswa atulie ili amalize kwanza tatizo lake la kesi, angetuliana mwisho angeweza kupata busara ya kufanya zaidi ya vile alivyofanya, mimi namchukulia kama mtu aliyechukua uamuzi huu kwa haraka,” alisema Dude.

Baby Madaha

BABY MADAHA, ISABELA MPANDA…

Mastaa wawili ambao ni marafiki ‘chanda na pete’, Baby Joseph Madaha na Isabela Mpanda, walimuunga mkono Wema, wakisema ameusikiliza moyo wake, kwani hivyo ndivyo wanavyofanya watu wote wanaojitambua. “Hata mimi huwa nausikiliza moyo wangu, ukiniambia fanya hivi nafanya, kwa sababu hakuna mtu anayetambua machungu yangu zaidi ya mimi mwenyewe, ninaunga mkono uamuzi wa Wema, ni mzuri na lazima tumuunge mkono,” alisema Baby Madaha.

“Nadhani ni makosa kufikiri kuwa Wema alichukua uamuzi ule kwa hasira, hasira gani, kwani tangu akamatwe hadi aachiwe ni siku ngapi, sasa mtu unafikiri siku ngapi, mwezi mzima? Waache kumsakama mtoto wa watu, tuheshimu uamuzi wake,” alisema Isabela Mpanda.

Batuli

MASHABIKI LUKUKI NAO NJIA PANDA

Mashabiki mbalimbali waliohojiwa na Risasi Mchanganyiko juu ya tukio hilo, nao walionyesha mgawanyiko, baadhi wakimuunga mkono na wengine wakimpinga, kitu kinachoonyesha kuwa kuna mpasuko mkubwa katika tasnia hiyo ambayo haifanyi vizuri kwa sasa.

 

 

Comments are closed.