The House of Favourite Newspapers

Lwandamina Awaongezea Makali Chirwa, Tambwe

STORI: Na Wilbert Molandi | CHAMPIONI

DAR ES SALAAM: WAKIJIANDAA kuwavaa Ngaya de Mbe ya Comoro Kocha Mkuu wa Yanga Mzambia, George Lwandamina, ameiangalia safu ya ushambuliaji na kubaini upungufu na jana alianza kuisuka upya.

Yanga, wanatarajiwa kuvaana na Wacomoro hao katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mchezo utakaopigwa nchini Comoro. Katika mechi hiyo, kama Yanga ikifanikiwa kuwaondoa Wacomoro hao, basi hatua ya pili itacheza na APR ya Rwanda au Zanaco ya Zambia.

Katika mazoezi ya jana asubuhi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Lwandamina alionekana akiikazania safu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Katika mazoezi hayo, kocha huyo alianza program zake kwa wachezaji kukimbia mbio fupi na ndefu, kuruka koni kabla ya kuhamia kwenye program ya umaliziaji.

Lwandamina, alionekana akiwapa mbinu mbalimbali za ufungaji washambuliaji wake, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe, Anthony Matheo, Juma Mahadhi na Emmanuel Martin. Akiendelea na program hizo, kocha huyo aliwapanga wawili wawili na kuwapa mpira mmoja washambuliaji hao kisha kuwataka waipite safu hiyo ya ulinzi kabla ya kufunga mabao.

Katika zoezi hilo, winga Simon Msuva pia alikuwa akifanya mazoezi ya kuwapigia krosi washambuliaji hao ambao walikuwa wakifunga kwa kuziunganisha langoni.

Wakati mazoezi hayo yakiendelea, mabeki wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Andrew Vicent ‘Dante’ na Pato Ngonyani walionekana imara kutokana na kutokubali kuruhusu mabao golini kwao jambo ambalo mara kwa mara lilikuwa likimfurahisha kocha huyo.

Save

Save

Comments are closed.